Timu ya Vijana ya Kenya, imefuta ziara yake ya
kwenda Dar es Salaam kwa ajili kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa
dhidi ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa
jina la Serengeti Boys.
Mchezo huo ulipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 23, 2016.
Kwa mujibu wa barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Robert Muthomi kwenda
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kufuta kwa ziara hiyo
kunatokana na nafasi ambayo Kenya imeipata.
Timu ya Taifa ya Vijana ya Kenya imeteuliwa
kushiriki michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la COSAFA
inayotarajiwa kuanza Julai 22, 2016 hadi Julai 31, 2016 mara baada ya
Msumbiji kujitoa kwenye mashindano hayo.
“Tunaomba kukutarifu kuwa timu yetu imetuliwa
katika michuano ya vijana ya COSAFA, hivyo ziara yetu Tanzania
haitakuwako kama ambavyo sisi wenyewe tuliomba mchezo huo kwenu (TFF)
ufanyike Julai 23, 2016,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na
Muthomi.
Licha ya kwamba mchezo huo hautakuwako, ratiba ya
Serengeti Boys ambayo inapambana kuwania nafasi ya kucheza Kombe la
Mataifa Afrika hapo mwakani, imebaki vilevile kwa timu kuingia kambini
Jumapili Julai 17, 2016 kwenye Hosteli za TFF zilizoko Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inayonolewa na Bakari Shime itapiga
kambi ya wiki moja katika hosteli hizo, kabla ya kwenda Madagascar
ambako itapiga kambi ya takribani wiki mbili ikiwa ni ahadi ya Rais wa
TFF, Jamal Malinzi ambaye alitoa ofa hiyo baada ya kuwatoa Shelisheli
kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa.
Serengeti Boys inatarajiwa kucheza na Afrika
Kusini kati ya Agosti 5, 6 au 7, 2016 huko Afrika Kusini kabla ya mchezo
wa marudiano utakaofanyika saa 9.00 alasiri, Agosti 14, 2016 kwenye
Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.
EmoticonEmoticon