Waziri
Mkuu, Kassim Majliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu wa Kanisa
katoliki katika sherehe za kumsimika Askofu wa jimbo la Geita, Flavian
Kassala (kushoto kwake) zilizofanyika kwenye kanisa kuu katoliki mjini
Geita Juni 12, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika kukabiliana
na changamoto mbalimbali zinazoikabili zikiwemo za rushwa, ufisadi na
matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema siku zote kumekuwa na
ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Asasi mbalimbali ikiwa ni pamoja
na madhehebu ya Dini katika kuwapatia huduma za kijamii kama vile, afya,
elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyingi nyingine.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema
hayo leo mchana (Jumapili, Juni 12, 2016) wakati alipomuwakilisha
Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli katika Ibada ya kuwekwa wakfu na
kusimikwa kuwa Mhashamu Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa
Jimbo Katoliki Geita.
“Serikali inatambua jitihada
kubwa zilizowekwa na Kanisa Katoliki katika Jimbo hili la Geita na
Tanzania kwa ujumla hivyo wito wangu kwa Baba Askofu na Waumini wa
Kanisa kwa ujumla wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya kutoa
huduma muhimu kwa jamii,” amesema.
Amesema maendeleo ya nchi
yanawategemea wote hivyo ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali
utawezesha maendeleo ya Taifa kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha
wananchi wote.
Waziri Mkuu amesema jukumu la
Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia Mtanzania
kujikomboa na umaskini na kwamba kazi kubwa ya viongozi wa dini
kuunganisha jamii na wala siyo kuwatenganisha.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema
kinachotakiwa kufanywa na wote ni kumwuomba Mwenyezi Mungu awawezesha
kuwaelewa viongozi walioko madarakani na kutii maelekezo yanayotolewa
kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii mamlaka.
Amesema iwapo waumini watatii na
kuzingatia mafundisho ya kiroho yanayotolewa na viongozi wao wa dini ni
dhahiri kwamba yatajenga imani miongoni mwao na upendo utatawala katika
jamii nzima.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kushirikiana na Madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania
wote bila ubaguzi, hivyo aliwasihi waendelee kuwekeza katika huduma za
jamii ikiwemo Shule, Vyuo, Zahanati kwa kuwa wana jukumu la kushirikiana
kwa pamoja kujenga taifa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
aliwaomba wote kwa pamoja waunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt.
Magufuli katika kupambana na uzembe, ubadhirifu na wote wanao kiuka
maadili ya utendaji wa kazi.
Kwa upande wake Askofu Renatus
Nkwande wa Jimbo la Bunda ambaye alikuwa msimamizi wa Kitume Jimbo
Katoliki Geita amewaomba waumini kumpa ushirikiano Askofu mpya wa jimbo
hilo.
EmoticonEmoticon