Pichani Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Raisi
Muungano na Mazingira na Idara ya Mazingira ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar wakiwa ndani ya boti kuelekea mkoa wa
kusini Pemba kushiriki zoezi la uzinduzi wa kupanda miti ya mikoko (leo) Juni 4
Kushoto Naibu wa Waziri wa Wizara ya Nishati, Maji
na Mazingira wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Juma Makungu Juma,
akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mazingira na Muungano Mhe. Luhaga Mpina
(katikati) walipokuwa wakielea kupanda miti ya mikoko kisiwa panza kusini
Pemba. Kulia ni Muwakilishiwa mkuu wa Wilaya.
Walioinama (kulia) ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina akipanda mbegu za miti
ya mikoko katika eneo la kisiwa Panza ikiwa ni siku ya uzinduzi wa upandaji
miti hiyo kisiwani Pemba, kushoto ni Afisa Mazingira mkuu kutoka Ofisi
ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira bw. Cretus Shengena (Picha na
Habari zote na Evelyn Mkokoi).
Evelyn Mkokoi,Pemba
4/6/2016
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mb)
amewataka wananchi wa kisiwa Panza katika Mkoa wa Kusini Pemba, kukabiliana
na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutunza mazingira
hasa kwa kupanda miti ya mikoko kwa wingi,ili kunusuru kisiwa hicho
kumezwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari.
Mhe. Mpina ameyasema hay leo kisiwani Pemba alipozingua kampeni maalum
ya kupanda miti ya mikoko ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupanda
miti.
Awali Mhe. Mpina alisemakuwa, serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania imeweza kupata kiasi cha fedha shilingi milioni 165 maalum
kwa kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi kwa kujenga
kuta za fukwe za Ocean Road jijini Dar es Salaam,Pangani Mjini Tanga,
Kilimani mjini unguja na kisiwa Panza kisiwani Pemba.
Aliongeza kuwa, kiasi hicho cha fedha pia kimeanza kutumika katika
kampeni hiyo ya kitaifa ya kupanda miti kwa kupanda miti ya mikoko
katika eneo la kisiwa Panza na ambapo miti zaidi ya milioni Moja inatarajiwa
kupandwa katika eneo la hekta 238, kisiwani pemba, pamoja na zoezi hilo
kuzinduliwa leo kisiwani pemba, miti hiyo aina ya mikoko pia
inatarajiwa kupandwa katika maeneo ya kilimani mjini unguja,bwawani,tovuni,
micheweni na Rufiji.
Naibu Waziri Mpina aliongeza kwa kusema kuwa suala la mazingira si
suala la Muungano lakini serikali hizi mbili zimeona umuhimu wa kushirikiana
katika eneo hili ili kuweza kukabiliana kikamilifu na madhara na hasara
zitokanazo na athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kunusuru visiwa
hivi kumezwa na bahari.
Akitolea mfano wa shule ya msigi na sekondari kisiwapanza ambazo
zipo hatarini kumezwa, mhe Mpina aliongeza kuwa wataalam
wa masuala ya mazingira watafanya tathmini kikamilifu na kuona namna
gani serikali inaweza kuongeza mbinu zaidi za kushughulikia maeneo haya
hatarishi, ili maji ya bahari yasiweze kuingia katika maeneo ya makazi.
Naibu Waziri Mpina aliwasisitizia wananchi wa kisiwa panza kutunza
mazingira kwa kutokukata miti ovyo na kuchoma misitu na watunze na kuilinda
miti ya mikoko iliyopandwa ili kuweza kufikia dhamira ya kukinusuru
kisiwa icho kumezwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mazingira kutoka katika wizara ya
Ardhi,Maji,Nishati,na Mazingira wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Mhe.Juma makungu Juma amesema maeneo mengi ya Zanzibar yaliyopo pembezoni
mwa bahari yameharibiwa na shughuli za binadamu, hivyo upandaji wa miti
ya mikoko katika maeneo hayo utazuia adhari za mabadiliko ya tabia nchi
kwa makazi ya watu na mashamba ambayo yamepelekea watu kuanza kuhama
katika makazi yao na haya yote ni matokea ya vitendo vya wananchi.
Zoezi hilo la kupanda miti ya mikoko lililofanyika kisiwani pemba
limeenda sambamba na maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo
hufanyika tarehe tano Juni kila mwaka.