REA-VIJANA CHANGAMKIENI FURSA ZILIZOPO KWENYE NISHATI SAFI YA KUPIKIA

November 26, 2025




*📌 Ni kwenye utengenezaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya matumizi ya nishati safi*


*📌 Mafunzo kwa vijana na vikundi vya wanawake kutolewa sambamba na ugawaji wa machine za kutengeneza mkaa mbadala*


*📌Mkakati wa Mawasiliano kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wote mjini na vijijini kuhamasisha ajenda ya nishati safi ya kupikia*


Wakala wa Nishati vijijini (REA) imewataka vijana nchini na vikundi vya wanawake kuchangamkia mafunzo yatakayotolewa na REA ya fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia. kupitia  ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kununua mashine za kutengeneza mkaa mbadala pamoja na kutoa mafunzo ya kutengeneza mkaa mbadala kwa vikundi vya wanawake na vijana. 

Hayo yamesemwa leo Januari 26, 2025 Jijini Dar es salaam na Mhandisi wa miradi kutoka REA Bi. Raya  Majallah kwenye kipindi cha Power bank kinachorushwa na Bongo Fm ikiwa ni muendelezo wa kutembelea Vyombo vya Habari kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutoa elimu.

Bi Raya amesema, sambamba na hilo REA inaendelea na maandalizi ya miongozo itakayotumika kuvitambua na kuvichagua vikundi vitakavyonufaika na mradi huo.


Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano serikalini kutoka Wizara ya Nishati Bi Neema.Chalila Mbuja amesema kuwa ushirikishwaji wa wadau katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.



“Katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia wadau wa Mawasiliano ni watu muhimu ili kupeleka taarifa kwa watanzania na kwa wakati juu ya umuhimu wa mabadiliko kwenye ajenda hii sambamba na wadau wengine” Alisema Bi. Mbuja


Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea  kusimamia mkakati madhubuti wa Mawasiliano unaolenga kuhakikisha Watanzania wote wanapata taarifa sahihi juu ya umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi kama mkaa na kuni, na badala yake kuchagua nishati safi zinazolinda afya na mazingira.


“Ushirikiano na wadau ni muhimu sana katika kufanikisha mkakati huu. Tunashirikiana na taasisi, sekta binafsi, na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote nchini,” amesema Bi. Mbuja.


Kwa upande wake, Mhandisi wa nishati kutoka Wizara ya Nishati Benezet Kabunduguru amesema kuwa  kuwa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia umeweka dira sahihi ya kuhakikisha watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na inapatikana kwa gharama nafuu na kwa wakati ili kuhakikisha lengo linafikiwa ambalo  serikali imejiwekea.


Amewaalikka wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa kuwekeza kwenye Teknolojia na Vifaa vya Nishati safi ya kupikia ili viwafikie walaji kwa wakati, na ndio maana Serikali imeweka ruzuku kwenye mitungi ya gesi ili kuwarahisishia wananchi


Kwa ujumla, ziara hiyo imeendelea kutoa mwamko kwa wananchi kuhusu faida za nishati safi ya kupikia, ikiwa ni pamoja na kulinda afya dhidi ya moshi, kupunguza ukataji wa miti, kupunguza gharama za maisha, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kaya na Taifa kwa ujumla.


Mwisho

#NishatiSafiYaKupikia

#OkoaMazingiraOkoaMaisha

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »