Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba Madelu kesho Jumamosi Mei
14, 201 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda na Young Africans katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali ya Nchemba ambaye atakabidhi
Kombe kwa Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
msimu wa 2015/16, wageni wengi maalumu watakaokuwa kwenye mchezo huo ni
Mkurugenzi wa Vodacom, Ian Ferrao sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ya Kuu Tanzania Bara (TBLB).
Mchezo huo utafanyika kwa baraka
za TPLB baada ya maombi ya Young Africans kukubaliwa na Ndanda ambao
watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni.
Mara baada ya mchezo huo, Mabingwa
Young Africans watapewa Kombe la ubingwa, medali na fedha Sh
81,345,723; Mshindi wa Pili Sh 40,672,861; Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044
na Mshindi wa Nne atazawadiwa Sh 23,241,635.
Mcehzaji Bora atapewa Sh 5,742,940
sawa na Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa bora wa michuano hiyo
inayodhaminiwa na Vodacom, Bia ya Kilimanjaro, Azam, Startimes na NHIF.
Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 saw na Kocha Bora wakati timu
yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.
Young Africans ndiyo iliyoomba kwa
Ndanda kadhalika TPLB kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es
Salaam kwa kuwa inatarajiwa kusafiri kwa ndege Jumapili kwenda Angola
kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola
utakaofanyika ama Mei 17 au 18, mwaka huu.
Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF
imesema kwamba Young Africans watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa
mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
litakalotolewa na Nchemba ambaye mara nyingi anaonekna uwanjani.
Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara
toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu
inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo
kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika mazingira
haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa
kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo.
Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za yanga ambazo Ndanda na Bodi
wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es Salaam.
Tayari Rais wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameipongeza timu ya soka ya Young Africans
kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya
pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
Hii ni mara ya 26 kwa Young
Africans ambayo kwa sasa inacheza mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la
Shirikisho Barani Afrika, kutwaa taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu
Tanzania Bara mwaka 1965. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya
kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza
Young Africans kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu
Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom
2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais Malinzi baada ya Young
Africans kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine
15 zilizoshiriki ligi hiyo.
EmoticonEmoticon