📍"Afya Bora, Vipimo Sahihi, Maendeleo Endelevu!”
📍"Tupime Sahihi, Tulinde Afya, Tujenge Taifa!”
Na WMA - Manyara
Wakala wa Vipimo (WMA) imeshiriki katika mbio za hisani za Manyara Tanzanite Marathon zilizofanyika mjini Babati mkoani Manyara tarehe 22 Agosti, 2026, ambapo watumishi wa Wakala walishiriki mbio za kilomita 5 na 10.
Ushiriki wa WMA katika mbio hizo ulikuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Wakala na Mkoa wa Manyara, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya njema na matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Mgeni rasmi katika mbio hizo alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo, akimwakilisha Waziri Mkuu. Mhe. Sillo aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha mbio hizo, akieleza kuwa tukio hilo lina umuhimu katika kuhamasisha jamii na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga na watoto njiti.
Katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alieleza kufurahishwa na ushirikiano kati ya WMA na Mkoa wa Manyara, akisisitiza kuwa vipimo sahihi vina umuhimu katika nyanja mbalimbali za maisha.
Mhe. Sendiga alisema vipimo sahihi si muhimu katika shughuli za biashara pekee, bali afya njema na pia ni kipimo sahihi cha utekelezaji wa majukumu yetu kwa ufanisi na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Manyara Bw. Dennis Misango aliwahimiza wananchi na wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi katika shughuli zao, akieleza kuwa kufanya hivyo ni muhimu katika kumlinda mlaji na muuzaji.
Alisema matumizi ya vipimo sahihi yanasaidia kujenga uaminifu, usawa na haki katika shughuli za kibiashara, huku yakihakikisha kuwa maslahi ya mlaji na muuzaji yanalindwa.
Manyara Tanzanite Marathon 2026 imefanyika ikiwa na kaulimbiu “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto Njiti”, ikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum ya kuwahudumia watoto njiti.
Akihitimisha tukio hilo, Mhe. Queen Sendiga aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuchangia kufanikisha mbio hizo, akisema mafanikio ya tukio hilo yametokana na ushirikiano wa Serikali, taasisi mbalimbali, wafanyabiashara, wanariadha na wananchi.
Mhe. Sendiga aliwashukuru pia washiriki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Manyara kwa kujitokeza kwa wingi, akisema ushiriki wao umeongeza hamasa na kuonesha nguvu ya mshikamano wa jamii katika kuchangia maendeleo, hususan kuboresha huduma za afya kwa watoto njiti.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Manyara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha dhamira ya kuimarisha huduma za afya inafikiwa, huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa wananchi.







EmoticonEmoticon