Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino,
ameipongeza timu ya soka Young Africans ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.
Young Africans imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo,
lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.
Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, Infantino
ameelezea ubingwa wa Young Africans kwamba umetokana na kazi kubwa
inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na
mashabiki.
“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii
kuipongeza Young Africans na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya
makubwa. Taji la Young Africans ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani
ya Young Africans,” amesema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha
habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Young Africans.
Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi
nzima la ufundi, wachezaji, madaktari pamoja na mashabiki wote wa Young
Africans.
“Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru
Young Africans na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi
mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema
Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei 21, mwaka huu.
Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo
imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la
ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri
zawadi ya fedha Sh 81,345,723.
EmoticonEmoticon