KASTICO: ASIKITISHWA NA VIFO VYA WATOTO WAWILI TOMONDO UZI ZANZIBAR.

May 19, 2016

CAS 
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar  imewataka Wazazi, Walezi na Wazee kuwalinda watoto wao dhidi ya Mazingira hatari yanayowazunguka ili kuwaepusha na athari za vifo pamoja na ulemavu.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar, Mauldine Castiko wakati akiwafariji wahanga wa tukio la vifo vya watoto wawili waliotumbukia katika Kisima cha Maji na kupoteza maisha huko katika mitaa ya Tomondo Uzi, Unguja.
Alisema wazazi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuwa waangalifu katika mazingira wanayoishi kwa kuyaweka katika hali ya usalama ili kuwaepusha na madhara  watoto wadogo yanayoweza kuwasababishia vifo na hatari zingine zinazoepukika.
Castiko alitoa mkono wa pole kwa familia hiyo na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa watoto hao wasiokuwa na hatia.
Aliisihi familia hiyo kuendelea kuvumilia katika kipindi kigumu cha msiba huku watu waliohusika na uzembe wa kusababisha vifo vya watoto hao wachukue juhudi za haraka kwa kufunika Kisima hicho ili kisiendelee kuhatarisha maisha ya watoto wengine mtaani.
Alisema serikali imesikitishwa na tukio hilo la vifo vya watoto wasiokuwa na hatia na kuahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa familia hiyo.
Alizitaka mamlaka zinazohusika na masuala ya ulinzi wa Raia na Mali zao  kuendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili watu watakaobainika kuhusika kwa uzembe na tukio wachukuliwe hatua za kisheria.
“Familia, Ndugu na Jamaa wa marehemu nakupeni pole na kukuombeni muendelee kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Lakini pia nachukua fursa hii kuwaomba wazazi na walezi kuwa makini na watoto wenu hasa awa wadogo kwani mazingira wanayokuwa wakicheza mengi hayana usalama juu ya maisha yao.”, alisisitiza Waziri huyo na kuongeza kuwa serikali haitowavumilia watu wanaohatarisha maisha ya watoto kwa makusudi na hatakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Waziri huyo alifafanua kwamba Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 pamoja na Mikataba mbali mbali ya Kimataifa  inayohusika na Haki za Binadamu iliyoridhiwa na serikali ya Tanzania inatambua na kutetea haki za Watoto kuhakikisha wanapata ulinzi wa kuishi na huduma mbali mbali za msingi kama walivyo watu wengine.
Alisema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuhakikisha maisha ya watoto yanakuwa salama wakati wote wakiwa ndani na nje ya familia zao huku ikiimarisha sheria na miongozo ya kusimamia haki zao Kikatiba.
Alitoa agizo kwa wananchi wote wa Zanzibar wanaomiliki visima vya maji ama kuchimba mashimo mbali mbali yanayoweza kuhatarisha maisha ya watoto, kufukia ama kuvifunika visihatarishe maisha ya watoto wengine.
Aidha alisema jamii inatakiwa kuwa makini na watoto wadogo hasa kwa kipindi hiki cha maradhi ya miripuko ya Kipindupindu kwa kuwaepusha watoto wasile wala kunywa maji machafu na vyakula visivyokuwa salama kwa afya zao.
“ Kuna baadhi ya familia hawafutilii mwenendo wa watoto wao pindi wanapokuwa nje ya majumba yao kujua wanakula nini wala wanacheza katika mazingira gani hali ambayo inaweza kuwaweka katika mazingira hatarishi watoto wetu.”, alisema Waziri huyo.
Naye Mama mzazi wa watoto hao,  Mariam Hassan alishukuru ujio wa kiongozi huyo na kueleza kwamba vifo vya watoto hao ni pigo kubwa kwa familia yake.
Alisema kwamba watoto hao walikuwa mazingira ya mtaani wakicheza ambapo yeye alikuwa akiendelea na harakati za kuandaa chakula cha mchana ghafla majira ya saa 7:30 mchana akaambiwa kwamba watoto wake wamedondoka katika kisima cha jirani yao hapo mtaani.
Baada ya kupata taarifa hiyo alifika katika kisima hicho ambapo alikuwa watu mbali mbali wakiendelea na juhudi za kuokoa maisha ya watoto hao lakini walipotolewa walikutwa washafariki kwani haikujulikana wameingia wakati gani.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Yussuf Faki Juma mwenye umri wa miaka miwili(2) na Muhamadi Ali Abdallah umri wa mwaka 1 na miezi nane wote wakiwa watoto wa familia moja.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »