CCM Z’BAR YAWATAKA VIONGOZI WAKE KUPAMBANA NA UPOTOSHAJI.

May 28, 2016

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
…………………………………………
       CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaagiza  viongozi wake kuzisoma vizuri Katiba ya CCM, Kanuni za maadili na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ili wawe na uwezo wa kujibu hoja za baadhi ya watu wanaosambaza fitna na uzushi wa kukichafua chama hicho.
Kimesema kiongozi yeyote mwenye uwezo na uelewa mzuri juu ya miongozo hiyo hawezi kuyumbishwa na kauli na maneno ya mitaani badala yake atakuwa na msimamo imara wa kusimamia maslahi ya chama kupitia vikao halali.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akizungumza na viongozi mbali mbali wa Chama kuanzia ngazi za matawi hadi wilaya huko katika Wilaya ya Amani Kichama, Unguja.
Aliwasihi viongozi hao kutumia vikao halali vinavyokubalika kikanuni kujadili changamoto na kasoro zinazojitokeza ndani ya chama kwa lengo la kuepuka maneno ya mitaani yanayoweza kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya CCM.
Alisema baada ya chama hicho kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu kwa asilimia 91, kilichobaki kwa sasa ni viongozi na wanachama kushirikiana vizuri na Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kusimamia vizuri Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho yam waka 2015/2020.
 “ Sisi viongozi tukiendelea kuwa wamoja na wenye kushirikiana kwa lengo la kusimamia maslahi ya CCM kwa vitendo basi, naamini kwamba chama chetu nacho kitaendelea kuwa imara na kushinda kwa kila uchaguzi.
Pia tujue kwamba ushindi wa uchaguzi mkuu wa marudio ndio mwanzo wa kujipanga kimikakati kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, kwani hakuna muda tena wa kusubiri ni lazima tuwe karibu zaidi na wanachama wetu ambao ndiyo wapiga kura wetu.”, alisisitiza Vuai huku akiwasihi vuiongozi hao kusoma alama za nyakati kwa kutathimini changamoto na kasoro zilizotokea katika uchaguzi mkuu uliopita ili zisizokee tena katika uchaguzi ujao.
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliendelea kufafanua kwamba CCM ni chama chenye asili ya amani na utulivu na kinachoamini kwamba umoja na msikamano ndiyo fursa ya kuifikisha katika kilele cha Zanzibar na maendeleo endelevu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia suala la ajira, Vuai aliwashauri vijana kutokata tamaa kwani CCM inaendelea kuikumbusha serikali kutafuta njia mbadala za kuhakikisha vijana wenye sifa, vipaji,uwezo na maarifa ya ujuzi mbali mbali wa chama hicho wananufaika na matunda ya ajira kutoka serikalini ama sekta binafsi.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo, alilaani vikali kitendo cha Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika ziara yake ya Pemba cha kuwakataza wananchi hasa wafuasi wake wasilipe kodi na kuwapandikiza mbegu za chuki zinazolenga kuingiza nchi katika migogoro inayoweza kuathiri uchumi wa nchi.
Alisema kitendo hicho hakikubaliki kwani kinavunja sheria za nchi na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwa makusudi jambo linalotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria na vyombo vya dola kabla nchi haijangia katika machafuko.
“Sio kwamba serikali inamuogopa Maalim Seif bali inafanya kila jambo kwa kufuata sheria na Katiba ya nchi, lakini pia ni lazima tukumbuke kwamba hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria.”, alisema Vuai na kuwasihi wananchi hasa wafuasi wa CCM wasiwe na jazba na watulie huku wakisubiri mamlaka husika zichukue hatua kwa watu wanaovunja sheria za nchi.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Amani Kichama, Abdallah Mwinyi alimuahidi Naibu Katibu Mkuu huyo kuyafanyia kazi mambo yote yaliyotolewa kama nasaha na ushauri kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya chama hicho.
Nao baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali  waliohudhuria kikao hicho, wameelezea kuridhishwa kwao na mikakati mizuri iliyopo ndani ya chama itakayosaidia kufanikisha ushindi wa dola katika uchaguzi mkuu 2020.
Pamoja na hayo wameahidi kuendelea kuwa wamoja katika kulinda maslahi ya CCM kwani ndiyo chama pekee kinachojali na kuthamini utu wa wananchi kupitia kauli njema za kuhimiza amani na utulivu wa nchi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »