REA IMEFANYA KAZI KUBWA YA KUFIKISHA HUDUMA ZA NISHATI VIJIJINI -WAZIRI NDEJEMBI

November 28, 2025


*📌Asisitiza ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia*


*📌Mradi wa vitongozi 9,000 mbioni kuanza*


📍Dodoma


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kufikisha umeme kwenye vijiji na maeneo ya pembezoni mwa miji iliyopelekea kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.


Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 28, 2025 wakati Mhe. Ndejembi alipokutana na kuzungumza na Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini pamoja na utekelezaji wa Mkakati wa nishati safi ya kupikia katika kikao kilichofanyika Ofisi za Makao Makuu ya REA jijini Dodoma. 

"REA imefanya kazi kubwa na nzuri sana hapa nchini hususan katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji. Kipekee nachukua fursa hii kuipongeza sana Bodi ya REA, Menejimenti  na Wafanyakazi kwa ujumla kwa kufanya kazi kubwa ya kupeleka umeme katika vijijini vyote nchini, " Amesema Mhe. Ndejembi. 

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, umeme vijijini haukuwa kama ilivyo leo na kuna watu walidhani kwamba kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ni hadithi na haitowezekana lakini sasa vijiji vyote vimesambaziwa umeme hapa nchini na REA imefanya kazi kubwa.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameipogeza REA kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wengine wakiwemo TANESCO ambao kwa kiasi kikubwa wameshiriki katika kufikisha mafanikio ya Wakala katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini. 

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Matarajio amesema kuwa, REA ni taasisi inayohakikisha kuwa Watanzania waliopo maeneo ya vijijini wanapata nishati safi na bora ya umeme ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija kupitia nishati hiyo. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali Mstaafu, Mhe. Balozi Jacob Kingu amesema kuwa REB itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Waziri Ndejembi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za miradi ya umeme vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amesema kuwa vijiji vyote 12,318 tayari vimefikishiwa huduma ya umeme. 


"Ufikishaji umeme kwenye vitongoji hadi sasa ni 39,003 kati ya 64,359 sawa na asilimia 61, vitongoji 2,562 vipo kwenye miradi inayoendelea (Densification 2A, HEP I, HEP IIA, HEP Lindi), " Amesema Mha. Saidy. 


Halikadhalika mradi kusambaza umeme kwenye vitongoji (HEP 2B) wa vitongoji 9,000 utatekelezwa katika kila mkoa hapa nchini ambapo mradi utakuwa wa miaka mitatu na wateja  wa awali wanatarajiwa kuwa 290,000.


Kuhusu nishati safi amesema REA inawezesha na kuhamasisha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi vijijini na pembezoni mwa miji, miradi  hiyo inahusisha gesi asilia, LPG, majiko banifu na mifumo ya nishati safi katika taasisi.


Mwisho.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »