Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
imetoa motisha kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanawake
(Twiga Stars) wakishinda katika mchezo wake dhidi ya Zimbabwe
unaotarajiwa kuchezwa siku ya Ijumaa Machi 04, 2016 katika uwanja wa
Azam Complex Chamazi.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Annastazia Wambura alipotembelea kambi ya timu hiyo leo jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza na wachezaji wa Twiga Stars, Wambura amesema kuwa
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo wamekusanya shilingi
milioni 15 ambazo zitatumika kama motisha kwa wachezaji hao.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa iwapo timu hiyo itaibuka na ushindi
katika mechi yake dhidi ya Zimbabwe kila mchezaji atapata gawio la
shilingi laki tatu (300,000) kama motisha na kuongeza kuwa itafanyika
hivyo hivyo katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Zimbabwe.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa michezo kuzidi kujitokeza
na kuisaidia timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kwa wingi katika
mchezo wa Machi 04, 2016 dhidi ya Zimbabwe utakayochezwa katika uwanja
wa Chamazi.
Aliongeza kuwa msaada zaidi unahitajika ili kuiwezesha timu hiyo
kukidhi mahitaji yake muhimu,hivyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali
kutoa michango yao kupitia Twiga Special Fund, Akaunti na: 20110001677
iliyoko NMB tawi la Bank House jijjini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa ameipongeza
Serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha Twiga Stars inapata huduma
muhimu ikiwemo motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Mwesigwa pia amewapongeza wadau wote waliojitolea kusaidi timu hiyo
ambapo amesema kujitokeza kwa wadau hao kunaongeza morali ya wachezaji.
Msaada huo wa shilingi milioni 15 umetolewa na wadau watatu ambapo
mmoja aliyechangia shilingi milioni 3 aliomba jina lake lihifadhiwe,
wengine ni Kampuni ya ASAS shilingi milioni 2 na Mamlaka ya Udhibiti wa
Mawasiliano Tanzania (TCRA) shilingi milioni 10.
EmoticonEmoticon