Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesikitishwa na
taarifa za upotoshaji za chombo kimoja cha habari ambacho mmoja wa
watendaji alipata fursa ya kuhudhuria mkutano mkuu kama mgeni mwalikwa
uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Tanga.
Katika hali inayotia mashaka, siku mbili kabla ya mkutano huo, chombo
hicho kiliripoti kuwa wajumbe walikuwa wanalalamika kwa kutopelekewa
nyaraka zinazohusiana na mkutano, wakati ukweli ni kuwa nyaraka hizo
zilitumwa tangu mwezi Novemba 2015 zikiwa ni sehemu ya barua ya mwaliko
wa kikao. Hivyo isingewezekana mwaliko wa kikao ukapokelewa na nyaraka
zisiwepo. TFF inao ushahidi wa nyaraka hizo kuwafikia wajumbe wa mkutano
huo.
Katika toleo lake la leo chombo hicho kilidai TFF kupata hasara ya shilingi za kitanzania milioni 500.
TFF inaviomba vyombo vya habari kuacha kupotosha juu ya taarifa za
mkutano mkuu kuwa shirikisho lilipata hasara (loss) , TFF haifanyi
biashara yoyote mpaka kufikia kupata hasara, kilichotokea ni kuongezeka
kwa nakisi (deficit) katika bajeti ya mwaka 2014.
Matumizi yaliongezeka kutokana na kulipa madeni ambayo uongozi wa
sasa uliyakuta uliyosababisha hata basi la timu ya Taifa likamatwe,
kuwepo kwa michezo mingi ya timu za Taifa (Taifa Stars, Twiga Stars,
Serengeti Boys), gharama ambazo zilijumuisha kambi za maandalizi za timu
pamoja na safari.
Kwa kuwa TFF haifanyi biashara yoyote, matumizi yaliongezeka zaidi ya
bajeti iliyokuwa imeratajiwa na kufanya kuwepo na upungufu wa zaidi ya
milioni 490.
Aidha TFF imesikitishwa na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo
vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita, kuhusiana na suala la tiketi za
Elektroniki.
Ifahamike kwamba TFF ndiyo ilianzishwa matumumizi ya tiketi hizo
kabla hazijasitishwa na Serikali mwaka jana kutokana na kubaini
mapungufu katika utekelezaji.
TFF haijawahi kugomea kuwepo kwa mfumo huo wa ki elektorniki, na kwa
kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na
Michezo wanaendelea na mazungumzo juu ya mfumo huo.
Vikao vinaendelea kati ya Wizara na TFF ili kuona njia gani itaweza
kutumika katika uendeshaji wa kuingia viwanjani kw aka kutumia mfumo wa
ki elektroniki na kesho kutakuwepo na kikao Wizarani kujadili mradi huo.
TFF inatafakari juu ya hatua za kuchukua dhidi ya wanaotoa taarifa za upotoshaji huo.