DIWANI wa kata ya Mangaka Halima Mchoma akikabidhi vitabu kwa mmoja wa walimu wakuu wa shule za msingi nne za kata ya Mangaka hii leo kwenye viwanja vya shule ya msingi Mangaka.
DIWANI wa kata ya Mangaka jimbo la Nanyumbu mkoani Mtwara, Halima Mchoma amenunua vitabu 488 vya masomo ya sayansi na stadi za kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 1,157,000/= kwa wanafunzi wa darasa la nne wa shule za msingi za kata hiyo.
Shule zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na shule ya msingi Mangaka,Nahawara,Ndwika 2 na Mtokora ambazo zote ni kutoka katika kata ya Mangaka Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
Vitabu alivyovinunua diwani huyo ni pamoja na vitabu 388 vya somo la sayansi, vitabu 100 vya somo la stadi za kazi pamoja na boksi nne za peni zenye peni 400 ambazo watapewa walimu wa shule za msingi katani humo.
Diwani huyo ameamua kununua vitabu hivyo pamoja na peni kwa walimu wote wa kata hiyo kwa fedha zake za mfukoni kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kutoa elimu bila malipo.
Akizungumza leo wakati wa kukabidhi msaada huo kwa walimu wakuu wa shule hizo katika viwanja vya shule ya msingi Mangaka alisema ameamua kununua vitabu vingi vya sayansi kutokana na ugunduzi wa gesi mkoani humo ambao wengi wa wataalamu wanaohitajika ni wale waliosoma masomo ya sayansi.
Alisema kutokana na kero ya upungufu wa vitabu kwenye kata hiyo waliyokuwa wanailalamikia walimu ndicho kilichomsukuma kuamua kununua vitabu hivyo ambapo kwa sasa kila mtoto wa darasa la nne atatumia kitabu kimoja kama inavyotakiwa kitaalamu.
Mchoma alisema kwa vitabu vya awamu ya kwanza alivyonunua vina thamani ya sh.1.2 milioni na kwamba lengo lake kwa sasa ni kutatua changamoto zilizopo kwenye shule hizo ikiwemo upungufu wa madawati,matundu ya vyoo,vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za walimu.
“Nimeguswa na tatizo la wanafunzi wa kata yangu kutumia kitabu kimoja zaidi ya wanafunzi wawili…ndio maana nimeamua kununua vitabu hivi ambavyo kwa sasa naamini kila mwanafunzi anayesoma darasa la nne kwenye kata hii atatumia kitabu chake na nitafanya hivi kwa kipindi chote cha uongozi wangu ndani ya miaka mitano,”alisema Mchoma.
Alisema pia amefanya uamuzi huo baada ya kuguswa na namna walimu wa kata hiyo wanavyojituma katika kufundisha kunakopelekea shule za kata hiyo kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani mbalimbali ikiwemo yale ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2015.
Kwa upande wake ofisa elimu taaluma wa shule za msingi wilayani Nanyumbu Stephen Urassa alimpongeza diwani huyo kwa namna alivyoonesha njia na kwamba msaada huo umekuja wakati muafaka ambao wanafunzi wa darasa la nne wanajiandaa kufanya mitihani ya majaribio.
“Nimekuwa Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu tangu mwaka 2008…lakini sijawahi kuona kiongozi yeyote wa kisiasa akitoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi hivyo hii inaonesha ni kwa namna gani wananchi wa kata ya Mangaka hawakufanya makosa kukuchagua”.alisema Urassa.
Naye mratibu Elimu kata wa kata ya Mangaka Fidelis Hokororo alisema kata hiyo ina jumla ya wanafunzi 253 wa darasa la nne ambapo kutokana na msaada huo kwa sasa kila mwanafunzi wa darasa la nne atakuwa anatumia kitabu kimoja cha sayansi huku vitabu 135 vikiwa zidifu.
Alisema kwa upande wa vitabu vya stadi za kazi ambavyo ni 100 kwa wastani kila wanafunzi watatu watakuwa wanatumia kitabu kimoja na kwamba watatumia baadhi ya vitabu vilivyopo kwenye shule hizo ili kufikia lengo la kila mwanafunzi kutumia kitabu kimoja.
EmoticonEmoticon