MENEJA
wa hoteli za Zanzibar Ocean View Jacob Makundi (kulia), akimkabidhi
Mkuu wa Idara ya Michezo wa Vyuo vya Mafunzo Khamis Ali Machenga,
shilingi 5,000 zikiwa gharama za tiketi za mechi ya Ligi ya Mabingwa
Afrika kati ya klabu ya Mafunzo na AS Vita ya DRC itakayochezwa Februaei
13, 2016, ambazo zilikwishachapishwa na kuanza kuuzwa. Kampuni ya
hoteli za Zanzibar Ocean View imeamua kubeba gharama hizo pamoja na za
mechi ya JKU na Gaborone United ya Botswana kuwania Kombe la Shirikisho.
(Picha na Ameir Khalid).
……………………………………………………………………………..
Na Salum Vuai, ZANZIBAR
UONGOZI wa kampuni ya hoteli za
Zanzibar Ocean View (ZGH), umeamua kubeba mzigo wa gharama za mechi za
wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya klabu barani Afrika
zitakazochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Mechi hizo za kwanza za raundi ya
awali, ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Mafunzo wataikaribisha
AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na JKU dhidi ya Gaborone
United ya Botswana.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo Februari 6, 2016 katika ukumbi wa Nyerere ulioko hoteli ya Zanzibar
Ocean View mjini hapa, Meneja wa hoteli hizo Jacob Makundi, amesema
hatua hiyo inalenga kuwafanya mashabiki wafike kwa wingi uwanjani siku
ya mechi hizo.
Alifahamisha kuwa, tayari kampuni
yake imezinunua tiketi elfu kumi (elfu tano kwa kila mechi) zilizobaki
baada ya nyengine kuuzwa, kwa gharama ya shilingi elfu kumi, na
zitagaiwa kwa mashabiki watakaofika uwanja wa Amaan siku za michezo hiyo
bila malipo yoyote.
Makundi alifahamisha kuwa, kampuni
yake pia itatoa fulana maalumu kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo,
ambazo watavaa kabla ya mechi ya kwanza na watakaposafiri kwenda DRC na
Botswana kwa ajili ya michezo ya marudiano.
Meneja huyo amezitaja gharama
nyengine ambazo kampuni hiyo itazibeba, ni kutoa punguzo la asilimia 75
kwa waamuzi, makamisaa, viongozi na wachezaji wa timu za wageni kwa
huduma ya malazi na chakula kwenye hoteli zake.
Ili kuwapa nguvu wachezaji wa
Zanzibar, Makundi aliahidi kuwa kampuni hiyo itatoa zawadi ya shilingi
milioni tano iwapo timu itashinda hapa nyumbani, na kuongeza kuwa
ushindi huo utakuwa chachu kwao kufikiria motisha zaidi kwa mechi za
ugenini.
“Kwa kuwa sisi ni wadau wakubwa wa
michezo, tumeona iko haja ya kuwashajiisha wawakilishi wetu hawa ili
wafanye vizuri na kuinua jina la Zanzibar katika soka la kimataifa na
tunatoa wito kwa taasisi nyengine zijitokeze kuongeza nguvu,” alieleza.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza
la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Khamis Abdallah Said, aliushukuru
uongozi wa kampuni hiyo, akisema unaonesha uzalendo kwa nchi katika
kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo.
Naye Abdallah Juma Mohammed,
aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo yenye hoteli tano kubwa
Unguja na Pemba Amani Ibrahim Makungu, alisema Zanzibar Ocean imeanza
lakini mlango uko wazi kwa wengine kuzisaidia timu hizo na pia michezo
mingine.
Akitoa shukuani kwa niaba ya timu
zote mbuli, Mkuu wa Michezo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKU) Khamis
Mohammed Suleiman, alisema ufadhili waliopata utawatia nguvu ya
kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Zanzibar kwenye michuano
hiyo.
Jumamosi Februari 13, Mafunzo
wataikaribisha AS Vita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa, wakati siku
inayofuata JKU watakuwa wenyeji wa Gaborone United kutika Botswana
kuwania Kombe la Shirikuso.
Mechi zote hizo zitachezwa katika
uwanja wa Amaan mjini Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni, na zile za
marudiano zitapigwa wiki mbili baadae.