Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo ametaka kasi iongezwe katika
mradi wa ujenzi wa kiwanda cha uchakataji na usindikaji wa gesi
kimiminika unaotarajiwa kuanza mkoani Lindi mara baada ya taratibu za
maandalizi kukamilika.
Profesa
Muhongo alisema hayo katika kikao kwa ajili ya kujadili hatua
iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho
kilichoshirikisha watekelezaji wa mradi huo ambao ni Shirika la
Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na makampuni yanayojishughulisha na
shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
Makampuni
ya utafiti wa mafuta na gesi yanayotekeleza mradi huo ni pamoja na
Shell, Statoil, Ophir Energy, Pavilion na Exxon Mobil. Pia kikao hicho
kilishirikisha watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wakala
wa Jiolojia Tanzania (GST)
Mara
baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda
cha kuchakata na kusindika gesi kimiminika Profesa Muhongo alilitaka
shirika la TPDC kushirikiana kwa karibu na makampuni ya utafiti wa
mafuta na gesi yanayotekeleza mradi huo na kwa kasi ya haraka ili mradi
huo uweze kukamilika kwa wakati.
Profesa
Muhongo alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi hivyo ni vyema
watekelezaji wakachangamkia fursa hiyo ya ujenzi wa kiwanda cha
kuchakata na kusindika gesi kimiminika ambayo mahitaji yake ni makubwa
duniani hususan katika bara la Asia.
“Ifikapo
mwaka 2025 inategemewa kuwa mahitaji ya gesi duniani yatakuwa ni
kiasi cha tani milioni 440 kwa mwaka hususan katika nchi za Asia ambazo
ni karibu na Afrika, hii ni fursa ambayo tunatakiwa kuichangamkia ili
kuendana na soko itakapofika kipindi hicho,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo aliendelea kusema kuwa gesi ya kimiminika imekuwa na mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi zinazoendelea huku akitolea mfano
wa Algeria ambayo ni nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na kiwanda cha
kuchakata na kusindika gesi kimimika ambayo kwa sasa imepiga hatua
kubwa kimaendeleo.
Katika
maandalizi ya awali ya mradi huo, Profesa Muhongo aliagiza uundwaji wa
timu kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo ikishirikisha wataalam kutoka
Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi,
Wizara ya Fedha, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), taasisi
mbalimbali pamoja na wawakilishi kutoka katika makampuni yanatofanya
utafiti wa gesi na mafuta nchini ambayo ni mtekelezaji wa mradi huo.
Alisisitiza
kuwa ni vyema timu hiyo ikawa na wataalam wenye uzoefu mkubwa
watakaofanya kazi kwa weledi na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Aliagiza kuwa timu hiyo kukamilisha taratibu zote za maandalizi kabla ya mwezi Novemba, mwaka huu.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) Dkt. James Mataragio alisema kuwa shirika lake limekuwa
likishirikiana na wabia wa ujenzi wa kiwanda hicho katika hatua zote za
maandalizi ya awali na kuahidi kuongeza kasi ili kazi hiyo iweze
kukamilika kwa wakati.
EmoticonEmoticon