Siku 100 za Rais John Magufuli, Wagonjwa Muhimbili Wapata Dawa kwa Asilimia 96

February 10, 2016

muh1
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu mafanikio ya hospitali hiyo katika siku 100 za Rais John Pombe Magufuli tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
muh2
Waandishi wa habari  na Madaktari wakifuatilia mkutano huo leo.
muh3
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Museru akisisitiza jambo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye hospitali hiyo.
muh4
Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Museru akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwenye mkutano huo.
………………………………………………………………………………………………………………….
 Wagonjwa anaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hivi sasa wanapata dawa kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka kwenye maduka ya dawa yaliopo hospitali hapa.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya uongozi wa hospitali hiyo kuboresha mfumo wa Tehama katika utoaji na uagizaji dawa.
“Wagonjwa wanaokosa dawa kwenye maduka yetu, hospitali inanunua haraka ili mgonjwa apate dawa kwa wakati. Kwa sasa ukosekanaji wa dawa hospitalini umepungua kwa kiasi kikubwa sana kutokana na kuimarisha utendaji ndani ya hospitali,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru.
Hayo yamesemwa leo na Profesa Museru wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya hospitali hiyo katika siku 100 za Rais John Pombe Magufuli tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Profesa Museru amesema kwamba Katika muda wa kipindi cha miezi miwili Disemba 2015 na Januari 2016, hospitali imefanikiwa kulipa wafanyakazi malimbikizo ya madai yao ambayo walikuwa wakiidai hospitali hiyo kwa kipindi kirefu.
Malipo hayo ni malipo ya on call, malipo ya wauguzi ya usiku, malipo ya posho mbalimbali hasa kwa madaktari pamoja na kada nyingine za afya ambazo zinashughulika moja kwa moja na wagonjwa.
Amesema kwamba kutolipwa kwa malipo hayo kulishusha morali ya wafanyakazi kwa kiwango kikubwa na kupunguza kasi ya ufanyaji kazi na hivyo kusababisha kukosekana kwa tija katika utoaji wa huduma kwenye hospitali hiyo.
Katika hatua nyingine, Profesa Museru amesema kwamba mapato kwenye hospitali hiyo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 baada ya Disemba hospitali hiyo kuzalisha Shilingi bilioni 3.3 kutoka wastani wa shilingi 2.7 zilizokusanywa miezi mitano (Julai 2015 hadi Novemba 2015)
“Mwezi  Disemba mwaka jana  tulizalisha shilingi bilioni 3.3 na Januari 2016 tulizalisha shilingi bilioni 4.3,” amesema mkurugenzi huyo.
Akizungumzia mashine za CT-Scan na MRI, Profesa Museru amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli ilinunulia Hospitali hiyo mashine mpya ya CT-Scan yenye uwezo wa 126 slices.
“Uwapo wa mashine hii mpya umeongeza uwezo kwa kiwango kikubwa wa kupima wagonjwa wengi kwa wakati mmoja. Sasa tunaweza  kumpima mgonjwa mmoja tumbo na kifua kwa sekunde sita. Awali  tulikuwa tunapima wastani wa wagonjwa 20, lakini sasa tunapima wagonjwa wastani wa 50 ndani ya saa 24.
“Baada ya kuwapo kwa mashine hizi mbili za CT-Scan, Hospitali haitegemei tena kukosekana kwa vipimo vinavyohitaji mashine hizi. Aidha mashine hii mpya ambayo ni ya kisasa zaidi na yenye nguvu kubwa imewezesha kufanya vipimo vya kiutalaamu zaidi hasa kwa upande wa viungo vya ndani kama moyo, utumbo, ubongo na hivyo kupata majibu sahihi ya chunguzi na uhakika zaidi. Mashine hii mpya tangu ilipofungwa Novemba 26, 2015 hadi Februari 9, 2016 imepima wagonjwa 863,” amesema Profesa Museru.
Amesema kwamba baada ya mashine ya MRI kutengenezwa wagonjwa zaidi ya 2,200 wamepimwa na kwamba baada ya mashine ya CT-SCAN kutengenezwa wagonjwa zaidi 1,000 wamepatiwa vipimo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »