Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa, akizungumza na Wadau wa Sekta ya
Ujenzi kuhusu Kuungana na Kushirikiana katika kuboresha Miundombinu hapa
nchini katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng.Joseph Nyamhanga akizungumza kuhusu
fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu hapa nchini katika
Mkutano huo uliyohusisha sekta binafsi na Serikali kuhusu namna ya
kuboresha sekta ya Miundombinu.
Naibu Waziri wa Miundombinu wa
Japan Koji Yonetani akizungumza katika Warsha hiyo na kusema nchi yake
iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha Miundombinu hapa
nchini.
Watendaji na Wadau wa Sekta ya
Ujenzi wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika Mkutano wa Wadau wa
Sekta ya Serikali na Binafsi kuhusu Ubora wa Miundombinu nchini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa (Wa kwanza kulia) akiwa kwenye picha ya
pamoja na Naibu Waziri wa Miundombinu wa Japan Koji Yonetani(Wa pili
kulia) pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Eng.Edwin Ngonyani (Wa Pili kushoto).
…………………………………………………………………………….
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wadau wa Sekta ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kushirikiana na wakezaji kutoka nchini Japan
katika kuendeleza miradi mbalimbali ya ujenzi, usafirishaji na
mawasiliano nchini.
Akizungumza jijini Dar es salaam katika mkutano uliowakutanisha
wadau wa sekta hiyo kutoka nchini Japan na Tanzania, Waziri Mkuu
Majaliwa amesema ushirikiano huo utaleta tija kwa taifa kwani wadau wa
Sekta hiyo wataweza kujifunza masuala mengi kutoka kwa wataalam hao.
“China na Japan ni moja ya nchi zenye Wakandarasi wengi na
wazoefu katika sekta ya ujenzi, kushirikiana nao kutaongeza ushindani na
kupelekea kupata fursa ya uwekezaji ndani na nje ya nchi, amesema
Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyataka Makampuni yote yenye miradi ya
ujenzi nchini kufanya kazi vizuri na kumaliza kwa wakati katika kipindi
hiki ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema fursa ipo kwa Kampuni kutoka Nje ya nchi kufanya kazi na
Kampuni za ndani kwa lengo la kupata Zabuni ndani na nje ya nchi, mara
zinapotangazwa.
“Kutokana na uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi, hatuna budi
Makandarasi wetu kuungana na kufanya kazi kwa ushirikiano na wenzenu
kutoka nje ili kupata maendeleo katika Sekta hii”, alisisitiza Waziri
Mkuu.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani kwa niaba ya Waziri, Prof. Makame Mbarawa amewaomba
Wawekezaji, Wakandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kutumia fursa hiyo, kuungana na kutengeneza kampuni za ubia
baina ya nchi hizo mbili ili kuweza kujenga miradi mbalimbali ya
maendeleo nchini.
“Tumieni fursa hii kupata elimu na uzoefu na hata kuunganisha
Makampuni kwani wenzetu wa Japan wana uzoefu mkubwa na maendeleo katika
Sekta hii, ukilinganisha na sisi”, alisema Naibu Waziri.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa kupitia mkutano huo Wakandarasi
nchini wataweza kujifunza njia za kisasa ambazo zitasaidia katika
kuboresha Sekta ya Miundombinu na Mawasiliano.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Miundombinu kutoka Wizara ya
Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan, Bwana Takatoshi
Nishiwaki, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kukubali kushirikiana
katika kuendesha mkutano huo na wadau wa sekta ya ujenzi wenye lengo la
kubadilishana ujuzi na teknolojia kuhusu Miundombinu bora.
Mkutano huo wa siku moja umewashirikisha Wawekezaji, Wakandarasi
na na Wafanyabiashara kutoka nchini Japan na Tanzania walio katika
Sekta ya Miundombinu na Mawasiliano.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.
EmoticonEmoticon