Budapest, Hungary
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmound Thabit Kombo(Mb.) akiambatana na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri, ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Mradi wa Kutibu Maji wa wilayani Csepel jijini Budapest nchini Hungary ambapo Tanzania inaazimia kupanua wigo wa ushirikiano katika eneo hilo na Hungary.
Moja kati ya malengo ya kutembelea mradi huo ni kujionea kazi ya Kampuni ya VTK Innosystem ya nchini humo ili kubaini uwezo na utalaam wa kampuni hiyo katika kutekeleza miradi ya maji na kufahamu namna Tanzania inavyoweza kunufaika kwa kufanya nayo kazi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kombo na Mhe. Aweso wamejionea uwezo na utalaam mkubwa wa kampuni hiyo katika usafishaji maji ambapo VTK tayari imetekeleza miradi ya usafishaji maji katika mataifa mbalimbali ikiwemo Rwanda, Cabo Verde, Kenya na Indonesia.
Kampuni ya VTK inatarajiwa kutekeleza mradi wa usambazaji maji wa Biharamulo, utakaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Hungary kwa kiasi cha dola milioni 55.1. Vilevile, Mhe. Kombo ameikaribisha kampuni hiyo kutembelea nchini ili kuyatambua mahitaji mahususi ya maji na kutumia utalaam wao katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa maji.
Aidha, katika ziara hiyo ujumbe umejifunza na kuona njia za uzalishaji na kutibu Maji kwa njia ambapo Mradi huu unatibu maji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mionzi ya Ozone badala ya kemikali.
EmoticonEmoticon