WATAALAMU UDSM WAKUTANA NA VIONGOZI WA TBN

March 04, 2025

Dar es Salaam 


Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamekutana na baadhi ya viongozi na wajumbe wa Tanzania Bloggers Network (TBN) kwa mahojiano maalum yenye lengo chanya la kukusanya maoni yao ili kuimarisha masuala ya blogging, nchini.


Hatua hiyo ya kukusanya maoni imekuja kufuatia wataalamu hao kuagizwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ipo katika utafiti maalum kwa nia ya dhati kuboresha Sera na kanuni zake mbalimbali katika eneo hilo la majukwaa ya mtandaoni.


Kikao hicho kimefanyika kwa mafanikio katika ofisi za TBN zilizopo kwa Aziz Ali, Temeke, watafiti hao wamechukua maoni ya TBN Makao Makuu, wakisema pia watafika katika Ofisi za Kanda za TBN.

Akizungumza Katibu Mkuu wa TBN Khadija Kalili amesema TCRA imefanya uamuzi sahihi kukutana na wadau wake kwa kupitia wataalamu hao kwani maoni yao yatawapa picha halisi juu ya tasnia ya habari na blogging kwa ujumla wake.


Amesema kilio kikubwa cha wana TBN ni gharama za usajili na tozo ya leseni kiasi ni kikubwa ambacho kwa uhalisia wengi bado hawamudu kulipia.


Amesema hali hiyo imefanya idadi kubwa ya wana TBN kushindwa kumudu kuendesha mitandao yao kutoka 300+ waliokuwapo kwanza hadi kufikia 100+ tu wanaoweza kulipia na kwa kusuasua.


Ameshauri pia TCRA kuendeleza utamaduni wa kukutana na wadau wake ikiwamo kwa mafunzo ya kuwaimarisha uwezo wao pamoja na kuangazia athari za gharama za bando za mtandao na vifaa.


Amesema ikiwa sekta ya blogging ndani ya tasnia ya habari ikisimamiwa vizuri kwa ushirikiano wa karibu na TCRA ni wazi kwamba Tanzania itanufaika na maudhui bora na yenye viwango ambayo yatasaidia kulinda maadili ya jamii yetu.


TBN yenye wanachama 300 waliopo wanaendesha mitandao kwa kusuasua kutokana na ada na tozo.


Watalaam hao walionesha kushangazwa na kuwapo kwa Chama Cha Bloggers chenye usajili kamili na wanachama zaidi ya 300, na pia wakaelewa bloggers ni tofauti na jumuiya zingine za waandishi wa mitandao ambao hawana blogs.


Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Siasa Mzenzi, Dkt. Patrokil Kanje , Dkt. Said Suluo.


Wengine ni Mjata Daffa , Ally Mshana na Viongozi na wajumbe wa TBN, wakiongozwa na Katibu Mtendaji Khadija Kalili , Beda Msimbe na Rahel Pallangyo.


Mwisho

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »