Ulinzi wa Tembo kwa kutumia Satelaiti waanza Ruaha

November 13, 2015

Shirika la Hifadhi za Taifa limezindua program maalum ambapo tembo 30 wanaoongoza makundi 30 katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha Rungwa watavalishwa kola malum shingoni zenye vifaa vinavyorekodi mienendo yao kwa kutumia satelaiti. Program hii inafadhiliwa kwa pamoja na taasisi za Global Environment Facility pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi alisema kuwa “ Lengo kuu la program hii ni kupata taarifa za kina juu ya mienendo ya tembo katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwa zitakazosaidia kubainisha maeneo ya shoroba na mitawanyiko kwa ajili ya ulinzi wa tembo”

UNDP kupitia ushirika wake na TANAPA/SPANEST wametoa kandarasi ya kazi hii kwa taasisi ya World Elephant Centre ya nchini Tanzania inayotarajiwa kuongeza hali ya usalama wa tembo hifadhini.

Teknolojia hiii inawezesha kujua mwenendo wa tembo ndani na nje ya hifadhi, kujua walipo, wanapopita, kasi yao ya kutembea, sehemu wanazojificha, wanazokunywa maji, wanazopumzika, maeneo wanayokaa kwa muda mrefu, kama wamekufa, wamejeruhiwa,wamehama hifadhi moja hadi nyingie na taarifa nyingine nyingi hivyo itakuwa rahisi kwa askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wao.

Kola hizo zenye uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mitatu bila kubadili betri zake zinafungwa kwa Tembo 30 wanaoongoza makundi 30.
Wataalam wa Uhifadhi wakiongozwa na Dk. Alfred Kikoti (wa kwanza kulia) wakiendelea na zoezi la uwekaji kola maalum kwa tembo zinazosaidia kudhibiti mienendo ya tembo ndani na nje ya hifadhi ya Mfumo wa Ikolojia wa Ruaha Rungwa.
Zoezi la uvalishaji wa kola maalum kwa tembo katika hifadhi ya Ruaha likiendelea.
Helikopta maalum inayotumiwa na madaktari kwa ajili ya kutambua na kupiga dawa ya usingizi kwa tembo kabla ya uvalishaji wa kola maalum.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (mwenye kofia) akishuhudia zoezi la uvalishaji kola maalum kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Daktari wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI) akijiandaa kumdunga sindano ya kumzindua tembo baada ya kukamilika kwa zoezi la kumvalisha kola maalum.
Picha ya pamoja ya wahifadhi walioshiriki zoezi la uzinduzi wa program maalum ya uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa wakati wa zoezi la uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.

Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
Baruapepe: dg@tanzaniapaks.com
Wavuti: www.tanzaniaparks.com

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »