NHIF YAMKABIDHI MKUU WA MKOA WA TANGA MWANTUMU MAHIZA MASHUKA 150

November 12, 2015
Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza
akipokea mashuka 150 kutoka kwa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoani Tanga,Ally Mwakababu kwa ajili ya vituo vitatu vya Afya,Maramba,Mkinga na Lanzoni vilivyopo wilayani Mkinga mkoani
hapa







 Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza akiwa kwenye
picha ya pamoja na viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) mkoani Tanga ofisini kwake mara baada ya kupokea mashuka 150 kwa ajili ya vituo vitatu vya Afya,Maramba,Mkinga na Lanzoni vilivyopo wilayani Mkinga mkoani hapa kulia ni Meneja wa NHIF mkoa wa Tanga,Ally Mwakababu na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga,Salum Chima na anayefuatia ni Afisa Matekelezo wa (NHIF) Miraji Msile


NA TANGA RAHA BLOG,

MKUU WA Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani hapa kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)ili kuweza kuongeza wigo mpana wa wanachama ambao wataweza kunufaika na huduma zao

Alitoa wito huo jana wakati akipokea mashuka 150 yaliyotolewa na mfuko huo vyenye thamani ya shilingi milioni tatu yaliyotolewa na Mfuko huo kwa ajili ya vituo vitatu vya afya vya Mkinga, Maramba na Lanzoni vilivyopo wilayani Mkinga ambavyo zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa mashuka.

Alisema kuwa endapo elimu itatolewa ya kutosha kwa wananchi wanaoishi maeneo mbalimbali mkoani hapa hasa wale wa vijijini itasaidia kuongeza idadi kubwa ya jamii inayoweza kunufaika na mfuko huo kwa ajili ya kupata matibabu.

  “Nisema kuwa pamoja na kazi kubwa mnayoifanya niwatake mhakikishe mnaendelea kutoa huduma nzuri kwa wanachama wenu ikiwemo kuhakikisha huduma za dawa hazikosekaniki kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuondoa usumbufu kwa wananchi “Alisema RC Mahiza.

Hata hivyo alisema kuwa msaada huo umefika wakati muafaka ambao wagonjwa na wananchi wanaokwenda kupata huduma kwenye vituo vya afya wanakumbana na changamoto ya uhaba wa mashuka hivyo itasaidia kupunguza makali ya kutokupatikana mashuka kwenye maeneo hayo.

  “Mimi binafsi ni mdau na balozi mzuri wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na nina vijana wangu sitini ambao watajiunga na mfuko huo kwa lengo la kuhakikisha wanapata matibabu wakati wanapougua kwa sababu maradhi yanatokea wakati wowote “Alisema RC Mahiza.

Kwa upande wake,Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga(NHIF) Ally Mwakababu alimueleza Mkuu huyo wa mkoa kuwa dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanasaidia huduma za afya kwenye maeneo yalikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa mashuka.

 “Mkuu wa mkoa sisi tumekuwa mstari wa mbele kuweza kusaidia harakati za kukabiliana na changamoto zinazopatikana kwa wananchi ambao wamejiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa kuhakikisha wanapata matibabu na dawa kwa wakati muafaka bila kuwepo vikwanzo vya aina yoyote ile “Alisema Mwakababu.

Aliongeza kuwa mikakati yao ni kuongeza ufanisi mkubwa katika
kuwahudumia wananchi waliojiunga na mfuko huo ili waweze kupata huduma za uhakika wakati wanapokuwa kwenye vituo vya afya ili kuepukana na usumbufu usiowa wa lazima

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »