Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 (U-15) leo
imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu, baada
ya kuichapa mabao 4-0 kombaini ya U-15 ya Tanga Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Ushindi huo umetokana na mabao mawili ya Issa Abdi dakika ya 21 na
23, Frank George dakika ya tisa na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 80.
Pamoja na ushindi huo, lakini vijana wa U-15 ya Taifa walikutana na
ushindani kutoka kwa wachezaji wenye vipaji wa U-15 ya Tanga.
Kivutio zaidi alikuwa ni kiungo Joseph Yakobo ambaye Tanga wanamuita
‘Sure Boy’ na mshambuliaji George Chande aliyeisumbua mno ngome ya timu
ya taifa iliyoongozwa na Nahodha, Maulid Lembe.
Wachezaji wote waliokwenda majaribio Orlando Pirates ya Afrika Kusini
mwezi uliopita, Asad Ali Juma, Issa Abdi Makamba, Kevin Deogratius
Kahego, Amani Amede Maziku na Athumani Maulid Rajab walicheza leo.
Huo unakuwa mchezo wa tano kushinda, kati ya mechi saba tangu kuundwa
kwa timu hiyo Aprili mwaka huu, ikifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa
mawili tu.
Timu hiyo iliifunga 4-1 na 3-0 Mbeya, ikaifunga 4-0 na 1-0 Zanzibar
na kutoa sare ya 0-0 na 1-1 na Morogoro kabla ya ushindi wa leo.
U15 inayoandaliwa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za vijana
Afrika mwaka 2017 nchini Madagascar zitakazoanza Juni mwakani, imekuwa
ikiweka kambi kila mwishoni mwa mwezi kwa ajili ya michezo ya kujipima
nguvu chini ya kocha Sebastian Nkoma.
Kesho U15 Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wake wa mwisho mjini
hapa, itakapomenyana na U-17 ya mkoa Tanga hapa hapa Mkwakwani.
Wachezaji wa kikosi cha U15 ya Taifa wote ni wanafunzi wa sekondari
mbalimbali nchini na ndiyo maana hukutanishwa mwishoni mwa mwezi tu kwa
mazoezi ya pamoja.