Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa
Selestine leo amesaini mkataba wa mwaka mmoja na mfuko wa huduma ya afya
(NHIF) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na
viongozi wa benchi la ufundi.
Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika katika hoteli ya Protea
Courtyard iliyopo Upanga jijini Dar es salaam ambapo katibu mkuu wa TFF,
Mwesigwa Selestine na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF Rehani
Athumani walisaini kwa niaba ya pande hizo mbili.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa uwekaji sahihi
mkataba huo, Mwesigwa amesema anaishukuru NHIF kwa kudhamini kutoa
huduma ya afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi kwa vilabu vyote 16
vinavyoshiriki Ligi kuu ya Vodacom.
Aidha Mwesigwa ameviomba vilabu vya Ligi Kuu nchini kutoa ushirikiano
na watoa huduma ya afya kwa wachezaji na viongozi kutoka NHIF pindi
watakapokuwa wanafika kwenye vilabu vyao kwa ajili ya shughuli
mbalimbali.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Rehani Athumani akiongea
kwa niaba ya mfuko huo amesema wako tayari kufanya kazi na kutoa huduma
ya afya kwa ngazi zote ikiwemo kwa timu za madaraja ya chini pia.
TFF na NHIF zimeingia mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini wa huduma ya
afya kwa wachezaji kwa ligi kuu na viongozi wa benchi la ufundi,
mkataba ambao unaeza kuongezwa kila unapomalizika.
TFF kwa kupitia bodi ya ligi inavitaka vilabu vyote vya Ligi Kuu
vitoe ushirikiano kwa wafanyakazi wa NHIF katika kurahisiha shughuli za
usajili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na nyaraka sahihi zikiwemo
picha za wahusika katika muda sahihi.