Na Profesa Mark Mwandosya
Katika
kipindi hicho nimekuwa nikitafakari maneno gani yanaweza kumwelezea Dr.
Abdallah Omari Kigoda, maneno ambayo yanaweza kumtendea haki, kuonyesha
masikitiko yangu na familia yangu, na kutoa pole kwa familia yake,
mkewe, watoto na ukoo wote wa Kigoda, wakiwa Handeni na popote
pengine.
Sijaweza kuyapata maneno hayo.
Kwani
yangekuwa maneno mengi, na yenye kubeba ujumbe mzito. Nakiri sina
umahiri wa lugha hasa katika kipindi cha majonzi. Neno kubwa na zito la
kiswahili ni POLE kwa wote, labda kuongezea uzito ni kusema POLE SANA.
Pole hizi pia ni kwa wana Handeni aliowatumikia kwa muda mrefu wa
maisha ya kazi; Mkoa wa Tanga, na wana Tanga, mliompa heshima ya uongozi
wa kisiasa na maendeleo ya jamii; jamii (fraternity) ya uchumi na
wachumi; na Watanzania kwa ujumla wetu.
Abdallah
Kigoda ni mmoja wa Watanzania wasomi na wenye uzoefu mkubwa na aliyetoa
mchango mkubwa kitaifa na kimataifa. Hakuwa mzungumzaji sana kama
ambavyo sisi wanasiasa tunategemewa kuwa. Alizungumza pale tu
ilipohitajika azungumze.
Kwa
wale tuliokuwa karibu naye tulishangazwa na kufurahishwa pia kwa majibu
yake mafupi, sahihi na ya kifalsafa, ya maswali magumu. Hakuna mtu
ambaye angaliweza kuuliza imekuwaje Kigoda amekuwa Waziri, imekuwaje
Kigoda amekuwa Mwenyekiti wa Kamati muhimu ya Bunge, au imekuwaje
amekuwa Mbunge wa Handeni kwa muda mrefu. Alikuwa anafaa, alikuwa na
uwezo na alikuwa anamudu majukumu yake.
Kati
ya mambo ambayo yalimnyima raha ni tatizo la maji Handeni.
Nathibitisha hilo. Kwani katika kipindi chote nikiwa Waziri mwenye
dhamana ya maji, hakuna siku ambayo tukikutana Bungeni, au katika Baraza
la Mawaziri, ambapo hakuniuliza, kunikumbusha, au kunisisitizia kuhusu
maji Handeni. Naamini waliofuata katika Wizara hiyo baada ya mimi
kuhamishwa, wamefuatilia suala hilo na ahadi zetu kwake na wanatekeleza
mpango wa maendeleo ya maji kuhusu Handeni. Kama bado basi njia bora ya
kumuenzi ni kutekeleza yale ambayo angependa kuyafanikisha alipokuwa
hai.
Kwa
kumalizia niwakumbushe tukio lililotokea wiki iliyopita la mitandao ya
kijamii kutangaza au kama watakavyosema leo kifo kutabiri kifo chake.
Miaka kumi iliyopita yeye na mimi tulikuwa katika “timu” ya watu kumi na
moja tulioomba ridhaa ya wana CCM ili mmoja wetu ateuliwe kuwa mgombea
wa Chama katika ngazi ya Urais. Kwa msemo wa kichama “Kura
Hazikutosha”!
Katika
kutafuta wadhamini tulikutana Mtwara, yeye akitokea Lindi. Taarifa
zisizo rasmi lakini zilizagaa siku moja kabla zilihusu Dr. Kigoda
kupoteza maisha!
Mithili
ya kukutana kwa Dr. David Livingstone na Henry Morton Stanley,Ujiji,
Kigoma, nikamuuliza “Bila shaka ni Dr. Kigoda”. "Naam", akanijibu kwa
kutabasamu.
Baada
ya mazungumzo mafupi akasema, “nawafahamu walionizushia kifo,
nimewasamehe”. Sio hilo tu alilokutana nalo katika mchakato ule, bali
kama alivyoniambia alikuwa "mhanga wa siasa za maji taka!” Na
waliomtakia kifo miaka kumi iliyopita! Msihofu. Kwani moyo wake ulikuwa
mkubwa. Alishawasamehe.
Kwaheri
Abdallah. Kama utumishi wa nchi ni vita, basi kama askari umepigana
vilivyo. Wakati wa kupumzika umewasili. Mwenyezi Mungu Airehemu Roho
Yako. Inna Lillahi wa Inna Ilahi Raji’un.
chanzo:blog ya wananchi
chanzo:blog ya wananchi