Picha mbali mbali za wajumbe na viongozi na wataalamu (washauri) kutoka shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) pamoja na wafanyakazi wa Tume ya nguvu za Atomiki Tanzania wakiwa katika semina ya juu ya usimamizi wa sheria na kanuni za usimamizi wa mionzi ya nyuklia Tanzania, iliyofanyika makao makuu ya Tume ya Mionzi Tanzania yaliyopo jijini Arusha. Picha na Yohana Challe. |
NA; YOHANA CHALLE ARUSHA.
TUME
ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), imesema kuwa imejiandaa vilivyo
katika usimamizi wa uchimbaji wa madini ya urani ambayo yanapatikana kwa
wingi hapa nchini.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia John Mngodo alisema
kuwa moja ya majukumu ambayo serikali inafanya ni kujiandaa juu ya
kusimamia uchimbajia wa madini hayo.
“Mkazo
uliowekwa hapa ni kwamba ni lazima usalama wa mionzi upewe mkazo hivyo
TAEC itahakikisha usalama unakuwepo na katika kila hatua ambayo watakuwa
wanajiandaa au wanachimba na kusafirisha madini ya urani lazima ukaguzi
ufanyike na kutoa kibali ili kuhakikisha usalama unakuwepo” alisema
Mngodo.
Mngodo
alizungumza hayo wakati wa kuhitimisha zoezi la kupitia taratibu za
uendeshaji, ukaguzi na usimamzi wa nyuklia na mionzi hapa nchini, zoezi
hili lilifanyika kwa siku kumi tangu Oktoba 4 hadi oktoba 14 mwaka huu
katika makao makuu ya Tume hiyo mkoani hapa kwa kushirikiana na
wataalamu kutoka zaidi ya nchi 10 duniani.
“Wataalamu
hawa walikuwa wakipitia taratibu na namna ya jinsi ambavyo
tunavyosimamia shughuli za mionzi na nyuklia hapa nchini” alisema
Mngodo.
Wataalamu
hawa wametokea katika nchi za Jordani, Irend, Ubelgiji, Sudani,
Kenya,Ukreini, Argentina, Australia, Pakistani, Nigeria, Zimbabwe,
Uingereza na Zambia
Wataalamu
hawa walikuja kwa mwaliko wa serikali ili kuweza kuisaidia Tume hii ili
kuweza kuboresha zaidi shughuli zinazoendelea hasa elimu kwa
wafanyakazi, pamoja na kupitia sheria na kanuni za usimamizi wa masuala
ya Nyuklia na mionzi hapa nchini.
Aliongeza
kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni jinsi ya kuwapata wataalamu
wa kusimamia shughuli hizo (rasilimali watu) pamoja na fedha, japo
akiipongeza serikali kwa kuendelea kujitahidi kutoa mafungu ili
kuendelea kuboresha shughuli za Tume.
Kwa
upande wake Leonard Kifanga ambaye ni Mwanasayansi mwandamizi wa
nyuklia, alisema kuwa lazima Tanzania iwe na mipango mikakati ya
kuboresha na kushughulikia ajali za kinyuklia zinazoweza kujitokeza,
kwani itasaidia kujiepusha na madhara ambayo yanaweza kuepukika kwa
urahisi na kwa haraka.
“Nashauri
lazima Tume na Taasisi za kusimamia majanga ziwe huru ili zifanye kazi
kwa uhuru zaidi na kwa haraka ili kila mtu aweze kuwajibika katika
nafasi yake na hii itasaidia kujua tatizo lilipoanzia” alisema Bwana
Kifanga.
Kifanga
ni mmoja wa waatalamu kutoka nchini waliokwenda japani kwenye uchunguzi
wa mlipuko wa kinu cha nyuklia cha Fukushima kilichotokea baada ya
kutokea tetemeko la ardhi lililoharibu mfumo wa kinu cha nyuklia na
hatimaye kinu kupasuka na kutokea mlipuko.