Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene (kulia) akifungua warsha kuhusu Dira ya Madini
Afrika iliyokutanisha wataalam kutoka taasisi za serikali nchini
lengo likiwa ni kuwapa uelewa juu ya sekta ya madini na usimamizi wa
mikataba. Katikati ni Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu na Mbadala
Mhandisi Edward Ishengoma. Kushoto ni mtaalam kutoka Kitengo cha
Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo.
Washiriki wa warsha kuhusu Dira
ya Madini Afrika wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi iliyokuwa
inatolewa na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (hayupo
pichani)
Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene (wa tatu kutoka kushoto; waliokaa mbele) akiwa
katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo kuhusu Dira ya Madini
Afrika iliyofanyika mjini Morogoro tarehe 21 Septemba, 2015.
…………………………………
Na Greyson Mwase, Morogoro
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wananufaika na
rasilimali za madini mbalimbali pamoja na gesi iliyogunduliwa kwa wingi
hivi karibuni, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka
taasisi za serikali watakaohusika na upitiaji wa mikataba yote ya
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta kabla ya
kusainiwa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene katika uzinduzi wa warsha kuhusu dira mpya ya madini Afrika
iliyofanyika mjini Morogoro.
Warsha hiyo ya siku tatu iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na
Madini ilikutanisha wataalam kutoka taasisi za serikali ikiwa ni pamoja
na Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais- Tume ya Mipango,
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na
Kijamii (ESRF)
Pia ilikutanisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini
pamoja na taasisi zake kama vile Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini
(TMAA), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Uendelezaji
Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mpango wa Kuongeza Uwazi na
Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Nchini (TEITI), Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Chuo cha Madini Dodoma
(MRI).
Simbachawene alisema uundaji wa timu ya wataalam mbalimbali kwa
ajili ya kupitia mikataba ya madini, gesi na mafuta ni moja ya
makubaliano katika utekelezaji wa Dira ya Madini ya Africa (Mining
Vision for Africa) iliyoasisiwa na wakuu wa nchi zenye madini katika
mkutano wake uliofanyika mwaka 2009.
Alisema kuwa katika kuhakikisha
kuwa sekta ya madini inachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za
Afrika zinazozalisha madini wakuu wa nchi walikubaliana kuanzishwa kwa
Dira ya Madini itakayowezesha sekta ya madini katika nchi wanachama
kuboreshwa na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi
Alisema kuwa katika utekelezaji wa Dira ya Madini ya Afrika,
nchi ya Tanzania imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam mbalimbali katika
taasisi za Serikali katika upitiaji wa mikataba hususan ya utafiti na
uchimbaji wa rasilimali za madini, gesi na mafuta.
Alisisitiza kuwa mara baada ya wataalam hao kupata mafunzo wataweza kupitia mikataba mbalimbali kabla ya kusainiwa.
“Ieleweke kwamba suala la mikataba litakuwa si kati ya watu
wawili bali wataalam watashirikishwa kwa kupitia mikataba hiyo na kutoa
mapendekezo yao kabla ya mikataba kusainiwa na Waziri ambaye ni
msimamizi wa sekta husika,” alisisitiza Simbachawene.
Akielezea ushirikishwaji wa wananchi katika usimamizi wa sekta
za madini, gesi na mafuta, Simbachawene alisema kuwa Serikali
imehakikisha kuwa mikataba yote inalenga kuwanufaisha wananchi kwa
kushirikishwa katika utoaji wa huduma katika sekta husika.
Akitolea mfano wa sekta ya gesi nchini, alisema fursa za utoaji
wa huduma zipo nyingi na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hizo
Hata hiyo alieleza kuwa Serikali ina mkakati wa kutoa mafunzo
kwa wanachi kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora ili ziendane na soko la
kimataifa.
“ Tunataka ifike mahali makampuni yanayofanya shughuli za
utafiti na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta yanunue huduma na bidhaa
kwa wananchi wa Tanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi,”
alisisitza Simbachawene.
Naye mtaalam kutoka Kitengo cha Nishati na Mabadiliko ya Tabia
Nchi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo
alisema kuwa shirika la UNDP limekuwa likishirikiana na Serikali katika
utoaji wa mafunzo kuhusu sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi
wa mikataba
Alisema sekta nyeti kama za madini, gesi na mafuta
zisiposimamiwa kikamilifu zinaweza kuibua migogoro badala ya kuleta
maendeleo.
Alisisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalam kutoka taasisi za
serikali wataweza kupitia mikataba mbalimbali ya utafiti na uchimbaji
wa madini, gesi na mafuta na kuishauri serikali kabla ya kusainiwa ili
kutumika rasmi.
EmoticonEmoticon