Na Semu Mwakyanjala, TCRA
KUMEKUWEPO na ukuaji mkubwa na
mpana wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania kwa upande wa miundombinu
na huduma ambavo kwa pamoja vimeleta faida kwa Watanzania katika miaka
ya hivi karibuni. Sekta hii inaongozwa na Sera ya Tekinolojia ya Habari
na Mawasiliano ( TEHAMA) ya mwaka 2003.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
kwa kifupi TCRA, ni chombo huru cha Serikali kinachohusika na kusimamia
sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini Tanzania na ina majukumu ya
kutoa leseni kwa makampuni ya mawasiliano, ikiwemo ya huduma za simu,
utangazaji, intaneti na posta na usafirishaji wa vifurushi.
TCRA ilianzishwa chini ya Sheria
ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania Na 12 ya 2003 ambayo iliziunganisha
zilizokuwa Tume ya Utangazaji Tanzania na Tume ya Mawasiliano Tanzania.
Tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake 1 Novemba 2003, TCRA iomekuwa
ikiwashirikisha wadau wake muhimu kupitia mashauriano kwenye masuala
mbalimbali.
Ukuaji imara na wa kasi wasekta
ya mawasiliano nchini ni sehemu ya matunda yanayoonekana na Serikali ya
Awamu ya Nne ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Sera nzuri za serikali na
kufunguliwa kwa soko huria zimewezesha kuongezeka kwa wawekezaji na
hivyo kuwapa watumiaji fursa ya kuchagua huduma bora wanayohitaji kwa
gharama wanazomudu.
Kuanzishwa kwa mfumo wa leseni za
muingiliano yaani (Convergence Licencing Framework) ambao ulianzishwa
mwaka 2005 kutokana na kuendelea kukua kwa kasi kwa teknolojia
kulikopelekea mwingiliano wa Teknolojia (Technological Convergence)
kumechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano.
Mfumo huu una aina nne za leseni ambazo ni:
- Leseni ya Mitandao (Network Facility):
Inajumuisha miundombinu
ya setelaiti, mitandao inayotumia waya aina ya optic fibre, uwekaji wa
nyaya na njia za mawasiliano, vifaa vya mawasiliano kutumia redio,
milingoti ya mawasiliano ya simu za mkononi, minara na vifaa vya
kurushia matangazo ya vyombo vya utangazaji;
- Leseni ya Mtandao wa Simu (Network Services):
Hii ni leseni inayoruhusu kutoa huduma za simu yaani sauti, picha na takwimu (voice, data, etc);
- Leseni ya Huduma (Application Services):
Hii ni leseni
inayoruhusu mmiliki kutoa huduma kama vile internet, kupiga simu kupitia
internet, takwimu kwa ajili ya biashara, na huduma za kutuma taarifa
fupi;
- Leseni ya Huduma ya Maudhui ( Content Services):
Hii ni leseni
inayoruhusu mmiliki kutoa huduma za utangazaji wa redio na televisheni
na taarifa kupitia mitandao ( online publishing) na taarifa za habari.
Leseni chini ya mfumo wa CLF
zinatolewa kwa ajili ya kutoa huduma katika ngazi nne- ngazio ya
kimataifa, ya kitaifa, ya mkoa na wilaya.
Maendeleo tunayoshuhudia kwenye
sekta ya mawasiliano nchini ni sehemu ya matokeo ya mpango mkakati wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wa 2006/7 hadi 2010/11 na 2011/12
hadi 2015/16 ambao ulibuniwa na kutekelezwa Menejimenti na Bodi ya
Wakurugenzi na kuwezeshwa na kuchangiwa na juhudi za watumishi wa
Mamlaka ambao wanafanya kazi kwa bidii na weledi.
TCRA inatekeleza mpango mkakati sambamba na dira,dhima au dhamira na lengo kuu la Mamlaka.
Dira ya TCRA ni “Kuwa Mdhibiti
mwenye hadhi ya kimataifa, kwa kuweka na kusimamia usawa katika haki na
majukumu ya watoa huduma za mawasiliano na kuendeleza huduma zinazojali
mazingira, na uwezo wa kiuchumi wa watumiaji.”
Dhima au dhamira ya Mamlaka ni
“Kuwa na mfumo mahsusi wa usimamizi, kuboresha utendaji wa watoa huduma,
na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kwa lengo la
kutoa mchango wetu kwa uchumi jamii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
Lengo kuu ni” Kuendeleza ustawi
wa Watanzania kupitia mfumo wa usimamizi wenye ufanisi na ambao
unawezesha kupatikana kwa huduma za mawasiliano kwa wote”.
Soko la TEHAMA limekuwa kwa
idadi ya watumiaji wa huduma hizo, kwa aina mbalimbali za huduma hizo na
kwa kuongezeka kwa eneo ambamo huduma mbalimbali zinapatikana; ingawaje
idadi ya watumiaji wa simu za mezani imepungua. Kuna laini za simu za
mkononi zipatazo 31,862,656 sasa ukilinganisha na laini 2,963,737 mwaka
2005. Watumiaji wa intaneti wameongezake hadi kufikia 11,000,000
Desemba 2014 kutoka 3,563,732 mwaka 2008. Kwa sasa, kuna hamu kubwa ya
matumizi ya intaneti na mwelekeo huu utaendelea; hasa kutakapokuwa na
ongezeko la mitandao inayowezesha kutoa huduma za intaneti; na
kuongezeka kwa mitandao ya jamii.
Sekta ya mawasiliano ni mojawapo
ya sekta zinazoajiri watu wengi zaidi. Matumizi a simu za mkononi
yamebadilisha mfumo wa maisha ya wananchi hapa nchini. Simu za mkononi
siio tu kifaa cha mawasiliano 9 kwa kuongea na kutuma ujumbe mfupi au
meseji0 lakini pia ni chombo cha kuimarisha watumiaji kiuchumi. Simu za
mkononi zina matumizi ya aina mbalimbali ya kijitali kama vile huduma za
fedha ambazo zinawawezesha watu kutuma na kupokea pesa. Watumaji wa
huduma za fedha kuopitia simu za mkononi hivi sasa wanaweza kununua
umeme, kulipia maji na kulipia huduma nyingine bila ya kuzalimika kwenda
nje ya nyumba zao.
Watumiaji wanaweza kutoa pesa
kwenye mashine za benki (ATM) na watu wengine wamejikomboa kutokana na
adha ya kukaa foleni ndefu na kupoteza muda ambao wangeutumia chini ya
mfumo wa zamani wa kibenki.