Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akisalimian na baadhi ya wananchi wa Mpanda waliofika kwenye ofisi ya
CCM ya Wilaya ya Mpanda kushuhudia na kumdhamini ilia pate sifa za
kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Juni 15, 2015.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akisalimiana na baadhi ya wanaCCM wa kijijini kwake Kibaoni wilayani
Mlele Juni 15, 2015 wakati alipokwenda kwenye Ofisi ya CCM ya kata ya
Kibaoni kabla ya kudhaminiwa na wana CCM wa kata hiyo katika nia
yake ya kutafuta uteuzi wa CCM wa kugombea urais katika uchaguzi uja.
Baadhi ya wananchi wa Mpanda
waliofika kwenye ofisi ya CCM ya wilaya ya Mpanda kumdhamini Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda katika nia yake ya kuwania uteuzi wa CCM kugombea
nafasi ya rais wa Tanzania Juni 15, 2015.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akiwapungia wanaCCM waliofika kwenye Ofisi ya CCM ya kata ya Kibaoni
kumdhamini katika nia yake ya kuwania uteuzi wa CCM katika kugombea
nafasi ya urais Juni 15, 2015.
(Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………….
WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda ambaye pia ametangaza nia ya kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amepata wadhamini 9,141 baada ya
kuhitimisha zoezi hilo katika mkoa wa Katavi.
Hadi jana mchana alikuwa
amekwishapata wadhamini 4,243 kwa kuzuru vituo viwili tu vya Inyonga na
Mpanda Mjini. Lakini hali ilibadilika alipofika kijijini kwao Kibaoni
kwenye ofisi CCM kata ya Kibaoni ambako alikuta maelfu ya watu
wakimsubiri ili wasaini fomu za kumdhamini.
Akitangaza idadi ya watu
walijitokeza kumdhamini Waziri Mkuu, Katibu wa CCM wilaya ya Mlele, Bw.
Sidael Goroi alisema kuwa tarafa za Mpimbwe na Mamba ambazo ziko kwenye
Bonde la Ziwa Rukwa zimetoa wadhamini 3,450 wakati tarafa ya Nsimbo
imetoa wadhamini 1,448 na kufanya jumla ya wadhamini 4,898 kwa jana
jioni tu. Tarafa ya Mpimbwe ambako Waziri Mkuu anatoka ina kata tisa
zikiwemo za Kibaoni, Mwamapuli, Ikuba, Usevya, Mbede na Majimoto.
Mapema jana asubuhi,
katika kituo chake cha kwanza cha Inyonga, yalipo makao makuu ya wilaya
yake ya Mlele, Waziri Mkuu alipata wadhamini 1,440. Alirejea Mpanda saa 9
mchana ambako katika ofisi ya CCM Wilaya alipata wadhamini 2,803 na
kufanya jumla ya wadhamini 4,243 kwa vituo hivyo viwili.
Akitoa nasaha zake kwa
wakazi hao jana jioni (Jumatatu, Juni 15, 2015), Waziri Mkuu
aliwashukuru wote waliomdhamini huku akiwaomba waendelee kumuombea
safari zote zilizo mbele yake na zoezi zima liende vizuri kwani suala la
urais siyo lelemama bali ni la kumtanguliza Mungu.
Akifafanua zaidi,
Waziri Mkuu Pinda alisema: “Suala la urais si la kufa na kupona bali ni
la kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwanza. Kila mgombea anapaswa amuombe
Mungu kwamba kama itampendezea na kumuona anafaa ndipo amchague yeye
(mtangaza nia).”
“Ndiyo maana mara zote
huwa nawaambia wenzangu kwamba hakuna haja ya kutukanana wala kupakana
matope. Huwa nawaambia tusikwaruzane wala tusitukanane kwa sababu hakuna
ajuaye Mwenyezi Mungu amemuandaa nani miongoni mwetu,” alisema.
Aliwataka wananchi na
viongozi wa wilaya hiyo watoe ushirikiano kwa wagombea wengine
watakaofika wilayani humo kuomba wadhamini.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JUNI 16, 2015.
EmoticonEmoticon