Na Masanja Mabula -Pemba
………………………………………
Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha amesema kuwa hakuna
mwananchi aliyetimiza sifa na masharti ambaye atakosa fursa ya
kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambalo limeanza
katika Wilaya ya Micheweni Pemba .
Amesema kuwa Tume
imendaa utaratibu ambao utawafanya wananchi wote waliotimiza mashari na
wenye vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi ambao hawajawahi kuandikisha
kwenye daftari kuandikishwa kwenye daftari hilo .
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi wakati wa zoezi hilo Wilayani hapa , Jecha
ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waliotimiza umri wa miaka kumi na
nane na ambao hawakuandikisha kwenye daftari kufika vituoni kwa ajili ya
kuandikishwa .
Amefahamisha kwamba
kujiandikisha katika daftari ni kutumia haki ya msingi kidemokrasia na
kikatiba hivyo ni vyema kila mmoja kuitumia haki hiyo ambayo itamwezesha
kupata fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka katika uchaguzi Mkuu
baadaye mwaka huu .
“Tume tumejipanga
vyema kwamba na kwamba hakuna mwananchi ambaye atakosa haki yake ya
kuandikishwa ambaye ametimiza masharti na vigezo , hivyo nawaomba
wananchi wajitokeze kwenye vituo vya kuandikisha ” alisema .
Aliongeza kwamba “Hii
ni haki ya kila kwa mujibu wa sheria na katiba kwani ndiyo inayompa
fursa ya kuweza kuchagua kiongozi anayemtaka na kwamba nawaomba sana
waitumie fursa hii ” alisisitiza Jecha .
Nao baadhi ya wananchi
waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wameipongeza tume ya Uchaguzi
kutokana na maandalizi iliyoyafanya kwani hakuna mwananchi ambaye
amelalamikia utaratibu huo .
“Utaratibu huu ni
lazima Tume tuipongeze kwani ni mzuri hakuna fujo , watendaji wake wako
makini cha msingi kila mwananchi mwenye sifa afike kuandikishwa katika
daftari ” alisema Raya Ali wa Micheweni .
Kwa upande wake Katibu
wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Khadija Nassor Abdi amewataka wanasiasa
kuacha kutoa vitisho kwa wananchi wenye asili ya Tanzania Bara ambao
wanataka kuwazuia ili wasijiandikishe katika daftari licha kwamba
wametimiza masharti na vigezo vyote .
“Tumebaini kuwepo na
njama zinazofanywa na wapinzani kwa kutaka kuwazuia ndugu zetu wenye
asili ya Bara hata kama wametimiza masharti , wanatishwa lakini sisi
tumeibaini na tunatoa wito kwa wanasiasa kuacha kupata uhuru ili watumie
haki yake kikatiba ” alieleza Khadija .
Awali Mbunge wa Jimbo
la Konde (CUF) Khatib Said aliwataka mawakala wa Chama hicho kuwawekea
pingamizi baadhi ya vijana wenye asili ya Bara akidai kwamba
hawajatimiza masharti ikiwemo umri wao .