MAREFA NA KATIBU ZFA WAITWA KUHOJIWA KWA TUHUMA ZA RUSHWA

June 04, 2015

Na Abdallah Salum, ZANZIBAR
SIKU mbili baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Sepp Blatter kujiuzulu kwa tuhuma za rushwa zinazowakabili maofisa sita wa shirikisho hilo, kadhia ya rushwa imetinga katika soka la Zanzibar.
Jana, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, imewaita na kuwahoji waamuzi watatu wa mpira wa miguu pamoja na Katibu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini Yahya Juma Ali kufuatia taarifa kwamba wamehusika na kupokea hongo.
Watu hao wanadaiwa kujipatia shilingi 110,000 kwa njia ya rushwa ili waipe nafasi  ya tatu timu ya Chuo cha Utumishi wa Umma (IPA) kwenye mashindano ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu yaliyofanyika mwezi uliopita.
Mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma katika mamlaka hiyo Shuwekha Abdallah Omar, akiwa ofisini kwake Mnazi mmoja, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni waamuzi, Mzee Nuhu Ali, Abdulrahman Mahfoudh na  Mohammed  Ali  Mohammed.
Aidha amemtaja Katibu Mkuu wa ZFA Wilaya ya Mjini, Yahya Juma Ali.
Ofisa huyo alisema mamlaka yake iliwakamata watuhumiwa hao ndani ya ofisi ya ZFA iliyoko katika uwanja wa Amaan, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema  siku moja kabla ya kukamatwa kwao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu Zanzibar (ZAHLIFE) Abdallah  Abdulrahman Mfaume, alisema jumuiya yao haijahusika na lolote kuhusiana na  rushwa katika mashindano hayo.
Hata hivyo, ametaka watu waliohusika na kadhia hiyo wachukuliwe hatua zinazostahiki.
Hadi mwandishi wa habari hizi akiondoka katika ofisi za ZAECA, watuhumiwa hao walikuwa wanaendelea kuhojiwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »