Balozi Seif Iddi afungua Semina ya usafiri wa Barabarani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar

June 06, 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifungua Semina ya siku moja ya Usafiri Barabarani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofanyika kwenye ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Juma Duni Haji akitoa maelezo kwenye Semina ya Usafiri wa Barabarani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kabla ya ufunguzi wa Senmina hiyo.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wadau wa usafiri walioshioriki semina ya usafiri wa bara barani wakifuatilia Horuba ya Mgeni rasmi Balozi Seif hayupa Pichani.
Mkurugenzi wa Idara ya Usafiri na Leseni Nd. Suleiman Kirobo akitoa Mada kwenye Semina ya Usafiri wa Barabarani iliyoshirikisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wadau wa sekta ya usafiri.
Mkuu wa Kikosi cha UsalamaBara barani Kamishna Msaidizi wa Polisi { ACP } Nassor Ali Moh’d akitoa ufafanuzi wa ajali za barabarani zinazoonekana kuongezeka kutokana na matumizi mabovu ya bara bara kwenye semina ya usafiri wa bara barani. Picha na – OMPR – ZNZ.

Viongozi wenye fursa za maamuzi pamoja na nyadhifa katika Taasisi za Umma Nchini wameombwa kuwaelimisha Vijana wao wanaoendesha vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani badala ya kuwasubiri kuwaombea wanapokamatwa na askari wa usalama bara barani kwa kufanya makosa tofauti ambayo mengi kati yao ni yale ya  makusudi.

Akiifunguwa Semina ya usafiri wa Barabarani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hapo kwenye ukumbi wa Baraza hilo Mbweni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema tabia ya baadhi ya viongozi kuwaombea Vijana wao kuwachiliwa kwa makosa yao ya makusudi ni kuwavunja moyo Polisi na kupelekea kuonekana hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Balozi Seif alisema imekuwa ni jambo la kawaida hivi sasa kwa baadhi ya Viongozi   kuwaombea vijana wao wasifikishwe Mahakamani  wakati wanapofanya  makosa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaondosha heshima yao ndani ya jamii.

Alisema uvunjwaji wa sheria za usafiri wa barabarani unaofanywa na watumiaji wa barabara hizo kama waendesha vyombo vya moto, gari zinazobururwa na wanyama, baskeli na ha waendao kwa miguu husababisha  ajali zinazoleta  madhara kwa Taifa.

Alisema jamii imekuwa shahidi iliwaona Vijana wanaoendesha Vyombo vya ringi mbili Vespa na Pili pili wakipakizana watu zaidi ya wawili katika chombo huku wakifukuzana kwa mwendo wa kasi wakiwa wamekaa katika mkao wao maarufu   { T. ONE } huku vyombo hivyo vikichomolewa breki kwa makusudi.

Alisema chakusikitisha zaidi baadhi ya vijana hao huendesha vyombo hivyo kwa ringi moja tuu vikiwa kwenye mwendo mkali bila ya hata kuvaa kofia ngumu lakini jambo  la ajabu zaidi baadhi yao ni viongozi katika Jamii hii.

Mapema Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mh. Juma Duni Haji  alisisitiza umuhimu wa mashirikiano ya pamoja kwa Taasisi zote zinazosimamia  shughuli na harakati za Bara bara ndio njia pekee itakayosaidia kupunguza au kuondosha kabisa changamoto ya usafiri wa Barabarani.

Wakitoa mada kwenye semina hiyo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu usafiri na usalama Barabarani Mkurugenzi wa Idara ya usafiri na Leseni Nd. Suleiman Kirobo, Mkuu wa Kikosi cha usalama Barabarani Msaidizi Kamishna wa Polisi ACP Nassor Ali Moh’d pamoja na Mdau wa Sekta ya Usafiri Bwana Waziri Hashim  walisema zipo sheria zilizopitwa na wakati mabazo kutofanyiwa marekebisho ya haraka zitaendelea kuchangia matatizo yanayopatikana katika matumizi ya usafiri wa Bara barani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/6/2015.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »