Na. Andrew Chimesela – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.
Rajab Rutengwe ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro
kutumia sheria zilizopo katika kusimamia vema suala la usafi wa
mazingira.
Dkt. Rutengwe
ametoa agizo hilo jana (19 Mei, 2015) wakati wa kikao maalum cha
uhamasishaji wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kilichofanyika
katika ofisi za mkoa huo.
Kiongozi huyo wa
ngazi ya mkoa alibainisha kuwa zipo baadhi ya sheria ambazo ni nzuri
na endapo zitafanya kazi mji wa Morogoro utakuwa safi muda wote kwani
sheria hizo zinaelekeza kila mwananchi kufanya usafi katika eneo
analoishi.
“Kila mwananchi
anatakiwa kufanya usafi wa mazingira umbali wa mita kumi kila upande
kutoka eneo analoishi, yaani mbele ya eneo lake, nyuma, kushoto na kulia
kwa eneo lake, sheria, taratibu na kanuni za usafi zisimamiwe
kikamilifu” alisema.
Aidha, Dkt.
Rutengwe alikwenda mbali zaidi ya kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa
mazingira na kutaka juhudi zaidi zifanyike ili kung’arisha mji wa
Morogoro hasa Manispaa ya Morogoro kwa kuwa Halmashauri hiyo ndio uso wa
mkoa wa Morogoro.
’’Ndugu wadau,
Mimi ninaheshimu sana mashindano haya lakini nimeona tuende zaidi ya
mashindano ya usafi kwa kulenga mambo makuu yafuatayo;
Kuufanya mji wa
Morogoro kuwa kijani wakati wote (Greening), Kuupendezesha mji wa
Morogoro wakati wote (Beutification) na Kuwa na uendelevu wa usafi baada
ya mashindano”, Dkt. Rutengwe alisisitiza.
Katika hatua
nyingine Dkt. Rutengwe amewaomba Wanahabari Mkoani humo kutumia taaluma
yao kuwaelimisha wananchi umuhimu wa usafi wa mazingira na hivyo
kuuboresha mji wa Morogoro huku akiwataka Wasanii ambao ni wazawa wa
mkoa huo nao wabuni na kutunga nyimbo zinazohamasisha, kuboresha na
kutangaza vivutio vilivyoko katika Mkoa wa Morogoro.
Naye Mstahiki
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Amir Nondo, alisema
katika kuendeleza Usafi wa mazingira wa Manispaa ya Morogoro muda wote,
kuna sheria ndogo ambazo wanazitumia.
Nondo
alibainisha kuwa moja ya sheria hizo ni kutoza faini ya shilingi elfu
hamsini (Sh. 50,000/=) kwa kila mwananchi anayekamatwa akichafua
mazingira kwa namna yoyote na faini hiyo anatozwa wakati huo huo.
Aidha, alisema
wanatoa motisha ya shilingi elfu ishirini na tano (Sh. 25,000/=) kwa
mwananchi yeyote atakayesaidia kukamatwa kwa wanaovunja sheria zilizopo
na kuchafua mazingira ya halmashauri hiyo,
Awali, wakati
akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kwenye kikao hicho, mbele ya wadau wa usafi
wa mazingira Ofisa Afya wa Mkoa wa Morogoro Bwana Carle Lyimo alisema, lengo
la kikao hicho ilikuwa ni kutoa mrejesho kwa viongozi wa Mkoa kazi
zilizofanyika kwenye Kampeini ya Usafi wa Mazingira katika Mkoa wa
Morogoro na kuongeza ushiriki kwa viongozi pamoja na jamii katika
utekelezaji wa Kampeini hiyo.
Aidha, kikao hicho kililenga
kujadili mikakati ya namna ya kuboresha usafi katika maeneo mbalimbali
ya Mkoa ili ifikapo wakati wa maadhimisho ya usafi kitaifa Mkoa uweze
kushika nafasi ya juu kitaifa.
Kwa Mkoa wa Morogoro
Halmashauri zote zimekuwa zikishiriki kwenye mashindano hayo isipokuwa
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo
ambazo zimeanza kushiriki kwenye mashindano hayo mwaka 2014/2015.
Takwimu zinaonesha Halmashauri
ya Manispaa ya Morogoro imekuwa na rekodi nzuri katika mashindano hayo
hususani miaka ya hivi karibuni kama inavyooneshwa hapa chini mwaka na
nafasi iliyoshika kwenye mabano;
Mwaka 2007
ilishika nafasi ya 18 kati ya Halmashauri 20, 2008 (15), 2009 (15), 2010
(12), 2011 (7), 2012 (12), 2013 (3) na 2014(3). mwaka 2015?
Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa
Mazingira ilizinduliwa na Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 5 Juni mwaka 2012 lengo likiwa
kuboresha miundo mbinu ya usafi wa mazingira katika ngazi ya kaya na
shule ili kuweza kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ambapo mashindano hayo ya Usafi Kitaifa yanatarajiwa kufanyika tarehe 5 Juni mwaka huu.
EmoticonEmoticon