NOOIJ AKALIA KUTI KAVU TAIFA STARS, MECHI 14 TIMU IMESHINDA TATU TU TANGU ATUE APRILI

May 19, 2015

Mart Nooij amekalia kuti kavu Taifa Stars
Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij anaweza kufukuzwa wakati wowote kuanzia sasa, kufuatia idadi kubwa ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutomkubali.
Nooij ameiongoza Stars katika mechi ya 14 jana tangu awasili mwishoni mwa Aprili kuchukua mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen na timu hiyo imefungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Kombe la COSAFA Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.
Matokeo hayo yanaiweka Stars katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali- baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.
Stars sasa lazima ishinde mechi zake mbili zijazo dhidi ya Lesotho na Madagascar ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.
Swaziland ambayo bao lake pekee lilifungwa na  Sifiso Mabila kwa shuti kali dakika ya 42 baada ya kutanguliziwa pasi kwenye njia na Xolani Sibandze aliyemtoka Oscar Joshua upande wa kushoto, waliizidi ufundi uwanjani Stars jana.
Stars ilicheza ovyo jana, mpango pekee wa kutafuta mabao ni kwa mipira ya kutokea pembeni, wakati huo huo timu ilitumia mshambuliaji mmoja tu, John Bocco ambaye muda mwingi alikuwa anakwenda kutafuta mipira pembeni.
Ilikuwa vigumu kuelewa Stars wanacheza mfumo gani jana, kwani pamoja na kuwa na viungo watatu uwanjani, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto na Said Ndemla, lakini bado timu ilikuwa haikai na mpira.
Mipira yote ilikuwa inapelekwa pembeni kwa mawinga akina Mrisho Ngassa na Simon Msuva wakampigie krosi Bocco aliyedhibitiwa vizuri na mabeki wa Swaziland.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kipindi cha pili, kwani Stars haikurudi na mpango mbadala- matokeo yake Swaziland wakang’ara zaidi uwanjani.
Mabadiliko yaliyofanywa na Nooij kipindi cha pili, yalikuwa kichekesho pia- kwani baada ya dakika 10 kipindi cha pili, Stars ilionekana kabisa ilihitaji kiungo mbadala wa Mwinyi Kazimoto, lakini Mholanzi huyo alimtoa Said Ndemla na kumuingiza Juma Luizio dakika ya 65.  
Maana yake alipunguza kiungo akaongeza mshambuliaji, lakini dakika 10 baadaye akapunguza tena mshambuliaji, Mrisho Ngassa na aliyeonekana kuwa muhimu zaidi uwanjani jana na kuingiza kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Kikosi cha Taifa Stars kilichofungwa 1-0 na Swaziland jana 

Mtu ambaye alitakiwa kumbadili mapema tu, pengine tangu mwanzoni mwa kipindi cha pili, Simon Msuva akamtoa mwishioni mwa mchezo dakika ya 82 akimuingiza Ibrahim Hajibu.
Pamoja na mapungufu ya wachezaji kutokana na nyota kadhaa wa timu hiyo kubaki Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali, ikiwemo majeruhi, lakini hata upangaji wa timu Nooij pia ulikuwa ni tatizo.
Bado kutoka wachezaji aliokuja nao hapa, angeweza kupanga timu tofauti na aliyopanga jana na ikacheza kwa uelewano mzuri na kupata matokeo mazuri.
Wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji wa TFF wanaamini Stars haipo katika mikono salama kwa Nooij na wanataka mabadiliko mapema kabla ya kuanza kwa kampeni za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika Juni.
Kuna wasiwasi hata juu ya mbinu za ufundishaji wa Nooij na ndiyo maana amekuwa hataki hata Waandishi wa Habari wa Tanzania wahudhurie mazoezi yake wala kupiga picha.
Mfumo pekee wa kushambulia anaofundisha mazoezini na kiungo kupeleka pasi pembeni, imkute winga apige krosi watu ‘wagombee goli’ na ndivyo hata Stars inavyoonekana kucheza sasa.
Utamu wa soka ya Taifa Stars umepungua kwa kiasi kikubwa kutoka ulivyokuwa chini ya kocha aliyetangulia, Kim Poulsen hadi Nooij na mchezo wa kesho wa COSAFA dhidi ya Madagascar unaweza kuamua hatima ya Mholanzi huyo.
Ingawa kuna imani kwamba, Nooij anapotoshwa na mtu wake wa karibu katika uteuzi wa wachezaji, lakini hata yeye mwenyewe kama kocha ni tatizo.
Katika mechi 14 ambazo Nooij ameiongoza Stars, imeshinda tatu tu, ikifungwa tano na kutoa sare mara sita, tena mechi nyingi ikicheza nyumbani.
TFF ilihadaika na wasifu mzuri wa Nooij aliyetua Tanzania akitokea klabu ya St George ya Ethiopia Aprili mwaka jana na kumpa Mkataba mnono.
Wasifu wa Nooij unasema amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12.
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kuhamia St George ya Ethiopia kabla ya kuja Tanzania Aprili mwaka jana. 
John Bocco pamoja na kuwa mshambuliaji pekee jana, lakini alilazimika kwenda pembeni kutafuta mipira jana

REKODI YA MART NOOIJ TAIFA STARS
Tanzania 0-0 Malawi (Kirafiki Mbeya)
Tanzania 1-0 Zimbabwe (kufuzu AFCON Dar es Salaam)
Tanzania 1-0 Malawi (kirafiki Taifa)
Tanzania 2-2 Zimbabwe (Kufuzu AFCON Harare)
Tanzania 2-4 Botswana (kirafiki Harare)
Tanzania 2-2 Msumbiji (Kufuzu AFCON Dar es Salaam)
Tanzania 1-2 Msumbiji (Kufuzu AFCON Maputo)
Tanzania 0-2 Burundi (Kirafiki, Bujumbura)
Tanzania 4-1 Benin (Kirafiki, Dar es Salaam)
Tanzania 1-1 Swaziland (Kirafiki, Mbabane)
Tanzania 1-2 Burundi (Kirafiki, Taifa. Stars Maboresho)
Tanzania 1-1 Rwanda (kirafiki Mwanza, Maboresho)
Tanzania 1-1 Malawi  (Kirafiki Mwanza, Stars kubwa)
Tanzania 0-1 Swaziland (COSAFA Rustenburg)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »