Na Anna Nkinda – Lindi
Vijana
mkoani Lindi wametakiwa kuwa wazalendo na kutobaguana bali wasambaze
upendo na kujiona wote ni sawa kwa kufanya hivyo wataondoa chuki na
kudumisha amani, mshikamano na umoja katika jamii inayowazunguka.
Mwito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua klabu zalendo zilizopo katika Manispaa ya Lindi.
Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kama
jamii itajenga tabia ya ubaguzi italeta chuki na upendo utatoweka na
hivyo kusababisha vurugu zitakazopoteza amani iliyopo.
Alisema
uzalendo ni kiini cha maendeleo hivyo huwezi kuwa mzalendo kama hupingi
rushwa na matumizi ya madawa ya kulevya, hutunzi mazingira, hushiriki
kuchangia utoaji wa damu salama na kutokuchangamkia fursa mbalimbali za
maendeleo zilizopo katika jamii yako.
Mama
Kikwete alisema, “Leo hii nimezindua klabu zalendo, Mzalendo ni mtu
mwenye huruma na mtu anayeona thamani ya kitu alichonacho tunzeni vitu
mlivyonavyo ikiwemo Amani ya nchi yetu na mjitoe kufanya kazi kwa bidii
ili muweze kupata maendeleo.
Aidha
Mama Kikwete aliwahimiza wanafunzi kujitendea haki kwa kusoma kwa
bidii hadi elimu ya chuo kikuu kwa kufanya hivyo wataweza kuajiriwa na
kujiajiri katika katika fani mbalimbali na kujiletea maendeleo katika
mkoa wao wa Lindi.
Akisoma
historia fupi ya klabu zalendo Mwalimu Mwajuma Malugu ambaye ni
Mwenyekiti alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuutetea na
kuulinda muungano wa Tanganyika na Zanzibari ndiyo maana wanatumia
namba za #26464#ikimaanisha tarehe 26 mwezi wa 4 mwaka 1964 siku ya
muungano.
Aliyataja
malengo mengine kuwa ni kuhamasisha wanafunzi na vijana waliopo mtaani
kuwa wazalendo na kuipenda nchi yao kwa kufanya hivyo wataepukana na
mambo yasiyofaa kwa maslai ya nchi yao.
“Mafanikio
tuliyoyapata ni kujenga umoja na ushirikiano, kuongeza idadi ya
wanachama na hii inatokana na kufunguliwa kwa matawi mengine ya uzalendo
mashuleni na mitaani, kuongeza na kupanua uelewa kwa wanafunzi na raia
kuhusu klabu ya uzalendo, kuwahamasisha watu kuwa wazalendo na kujitoa
katika uchangiaji wa damu, kupinga rushwa, madawa ya kulevya pamoja na
kulinda Amani ya nchi.
Mwalimu
Mwajuma alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uhaba wa
fedha kwa ajili ya kuandaa makongamao na mabonanza yatakayosaidia
kuimarisha harakati zote za klabu ya uzalendo na kushindwa kutuma
wawakilishi katika mikutano na makongamano ya wanaklabu ngazi ya taifa.
Pia kikundi kimekosa semina kwa wanaklabu hali inayoplekea wanachama kukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhumuni ya klabu hiyo.
Klabu
zalendo ilianzishwa na walimu wa Shule ya Sekondari Lindi katikati mwa
mwaka jana hadi sasa inawanachama 1450 kutoka shule za Sekondari Mkonge,
Angaza, Ngongo, Ng’apa, Chikonji, Mingoyo, Kineng’ene , chuo cha ufundi
VETA na walimu wa shule za msingi pamoja na wanafunzi wao.
Pia
klabu hiyo imehusisha vijana kutoka mtaani wanaofanya kazi za udereva wa
pikipiki maarufu kama bodaboda, wavuvi na wanavikundi vya Sanaa.
Mama
Kikwete aliahidi kukipatia kikundi hicho mipira 20 na jezi seti 10 kwa
ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ambao watashiriki
katika mashindano mbalimbali `na kuangalia utaratibu wa kuwapatia mradi
ambao utawasaidia kuwainua kichumi.