WANACHAMA arobaini na tisa waliohudhuria
mkutano wa klabu hiyo kati ya sabini na sita wa klabu ya African Sports juzi
walipitisha katiba mpya wa klabu hiyo ambayo itawapa dira kuu ya kuelekea
ushiriki wao katika Michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara .
Katiba hiyo inaendana na katiba
nyengine ya vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ikiwemo ile ya shirikisho la soka
hapa nchini ambapo ilipitishwa na wanachama hao kwenye mkutano wa wanachama wa
klabu hiyo ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Splended jijini Tanga.
Akizungumza mara baada ya kuipitisha
katiba hiyo, Mwenyekiti wa Klabu ya African Sports, Hassani Shehe alisema kuwa
wanamshukuru mungu kupitisha katiba hiyo ambayo ilikuwa ni muhimili mkubwa kwa
maendeleo ya timu yao baada ya kupanda daraja ya Ligi kuu.
Hassani alisema kuwa mkutano huo
ulikuwa na mambo muhimu mawili ambapo la kwanza lilikuwa ni kupitisha katiba
hiyo ikiwemo kukutana na wanachama kwa ajili ya kutambuana.
Alisema kuwa baada ya kumalizika
suala hilo muhimu kwao watajiandaa na taratibu wa uchaguzi mkuu wa viongozi
ambao wataiongoza klabu hiyo na usajili kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi kuu
hapa nchini.
Awali akizungumza katika mkutano
huo,Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga(TRFA),Salim
Omari aliwataka viongozi na wanachama wa klabu hiyo kuhakikisha wanashikamana
ili kurudisha makali ya timu hiyo ya miaka ya nyuma.
“Tunafahamu vizuri enzi za miaka ya nyuma timu hii ilipokuwa ikifanya
mambo makubwa katika michuano ya Ligi kuu hivyo viongozi hakikisheni hili
linajirudia msimu ujao lakini kikubwa kuweni na ushirikiano “Alisema Salim.