WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amesema mkoa wa Mbeya unaweza kupaa kiuchumi kama
utazingatia fursa za kibiashara ilizonazo na kuwekeza zaidi kwenye
viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na mifugo.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu,
Machi 2, 2015) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa
Mbeya waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara yake ya siku saba kwenye
mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.
“Nguvu kubwa mnayo katika biashara
hasa kama mtajitahidi kutumia vema fursa kubwa ya uwekezaji katika
viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo
mliyonayo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya
katika msimu wa 2013/2014 umeweza kuzalisha tani 4,159,907 za nafaka na
kuuwezesha kuwa na ziada ya chakula ya tani 3,347,680.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema
mkoa wa Mbeya bado una fursa nzuri ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara na unaweza kuiwezesha kama nchi kuuza chakula katika
masoko ya Afrika na Afrika ya Mashariki kama watajipanga vizuri.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
aliwapongeza viongozi hao kwa kuuwezesha mkoa wa Mbeya kutoa mchango
mkubwa katika Pato la Taifa. “Katika taarifa ya mkoa, nimeelezwa kuwa
mwaka 2013, mkoa huu ulichangia shilingi trilioni 3.951 na hivyo kushika
nafasi ya tatu kati ya mikoa yote nchini ikitanguliwa na mikoa ya Dar
es Salaam na Mwanza.”
Alisema kutokana na ukuaji wa kasi
wa idadi ya watu ambao ni asilimia 2.7, mtu akichukua pato hilo la mkoa
na kuligawanya kwa idadi ya watu wa mkoa wa Mbeya anapata wastani wa
pato la kila mwananchi kuwa ni sh. 1,420,427. “Kipato hicho, ni sawa na
shilingi 118,369 kwa mwezi au shilingi 3,946 kwa siku sawa na Dola za
Kimarekani (US $) 2.3,” alifafanua.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba mtu
akichukua wastani wa pato la kila mwananchi kwa mwaka 2013 na kupanga
kwa mikoa yote, mkoa wa Mbeya unashuka na kushika nafasi ya sita
kitaifa. Aliitaja mikoa inayowatangulia kuwa ni Dar es Salaam sh.
1,990,043/- ambao ni wa kwa kwanza; wa pili ni Iringa (sh. 1,660,532/-);
wa tatu ni Arusha (sh. 1,448,782/-); wa nne ni Kilimanjaro (sh.
1,444,882/-); wa tano ni Ruvuma (sh. 1,438,392/-) na wa sita ni Mbeya
(sh. 1,420,427/-).
“Nawashauri muongeze juhudi za
kuipita mikoa hiyo kwa kuwa mna fursa nyingi za kuongeza uzalishaji hasa
katika mazao ya kilimo cha kahawa, kakao, mpunga, mahindi, viazi,
pamoja na mazao ya maliasili kama vile mazao ya misitu, na uvuvi na
uchimbaji madini,”.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake
ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho ya ziara yake na
amerejea jijini Dar es Salaam jana jioni (Jumatatu, Machi 2, 2015)