Timu za Ujenzi Rukwa na Volcano FC
ya Morogoro zimeshushwa madaraja mawili hadi ligi za wilaya baada ya
kushindwa kufika uwanjani kwenye mechi zao za Ligi Daraja la Pili (SDL).
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya
Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
jana jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za matukio mbalimbali ya ligi
hiyo.
Ujenzi Rukwa ilishindwa kwenda
Kigoma kuikabili Mvuvumwa FC ya huko wakati Volcano FC haikutokea kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo ilitakiwa kucheza
na Wenda FC.
Uamuzi wa Kamati ya Mashindano
umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 27 ya SDL ambapo mbali ya kushushwa
madaraja mawili, lakini pia timu hizo zimepigwa faini ya sh. milioni
moja kila moja. Vilevile matokeo yote ya mechi zao kwenye Ligi hiyo
yamefutwa.
Nayo Singida United imepewa
ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Ujenzi Rukwa kubainika
kumchezesha mchezaji asiyestahili (non qualified) kwenye mechi
iliofanyika Februari 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mandela mjini
Sumbawanga na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Mchezaji Emmanuel Elias Mseja wa
Mbao FC amepigwa faini ya sh. 100,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya
kukojoa uwanjani kwenye mechi dhidi ya AFC iliyochezwa Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Pia viongozi wa Mbao FC, Abdallah
Chuma (Daktari) na Meneja Yasin Abdul wamefungiwa miezi sita na faini ya
sh. 100,000 kila mmoja kwa kumtukana na kumtishia maisha Kamishna wa
mechi hiyo.
Nayo klabu ya AFC imepigwa faini
ya sh. 300,000 kutokana na washabiki wake kuifanyia vurugu timu ya
Bulyanhulu FC kwenye mechi yao iliyofanyika Februari 7 mwaka huu Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid na kumalizika kwa sare ya bao
1-1.
Timu ya Magereza Iringa imepigwa
faini ya jumla ya sh. 200,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha
maandalizi ya mechi (pre match meeting), na uwanjani kwenye mchezo wao
na Njombe Mji uliochezwa Februari 21 mwaka huu. Naye mchezaji wa timu
Amasha Mlowasa amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 100,000 kwa
kumtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi hiyo.