WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amezindua Mpango wa Kitaifa wa Kukuza Stadi za
Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unaolenga kukuza viwango vya uelewa
kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili kwa nchi nzima.
Mpango
huo wa miaka mitatu ulioanza kutekelezwa 2014/2015 hadi 2016/2017
umelengwa kuwahusisha watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13 walio
kwenye mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi (MEMKWA).
Akizungumza
na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi walioshiriki uzinduzi huo jana
jioni (Jumamosi, Februari 7, 2015) Waziri Mkuu Pinda alisema mpango huo
ni mkubwa na umeandaliwa mahsusi kujibu changamoto zilizojitokeza miaka
ya nyuma.
Aliwataka
watekelezaji wakuu wa mpango ambao ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto kuhakikisha kuwa wanazishirikisha asasi zisizo
za Kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya elimu.
“Kuna
mashirika mengi yasiyo za kiserikali ambayo ni chachu ya kuhimiza elimu
nchini... jaribuni kuwashirikisha sababu wao ni wadau wazuri sana wa
suala hili. Pangeni utaratibu wa kukaa na hawa wadau na kuwapa mrejesho
wa mpango huu mzima,” alisema Waziri Mkuu.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wahusika wakuu wa mpango waangalie
mgawanyo wa mikoa iliyoingizwa kwenye mpango huo kwa kuzingatia kanda
ili kuleta matokeo ya mtawanyiko badala ya hali ilivyo sasa.
“Nimeangalia jinsi mlivyogawa mikoa yenu, inanipa taabu kidogo... kuna
mikoa inahitaji msukumo wa pekee, mikoa ya wadugaji, mikoa iliyoko pwani
ya bahari na maziwa, yote inahitaji msukumo wa tofauti,” alisema.
Katika
taarifa yao, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisema mpango huo wa
KKK au LANES (Literacy and Numeracy Support Programme) unafadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu (Global Partnership for Education – GPE) na wahisani wengine.
Wahisani
hao ni pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) kupitia mradi
wa EQUIP-T unaotekelezwa katika mikoa saba ya Kigoma, Shinyanga, Mara,
Simiyu, Lindi, Dodoma na Tabora; Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo ya Elimu kwa Mtoto (UNICEF) wanaofadhili utelekezaji wa Mpango
wa LANES katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe; na Shirika la
Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia Mradi wa TZ-21 unaotekelezwa
katika mkoa wa Mtwara.
Mapema,
akisoma taarifa ya mpango huo mbele ya Waziri Mkuu, Kamishna wa Elimu
nchini, Prof. Eustella Bhalalusesa alisema mpango huo umelenga kuongeza
ufanisi katika stadi za KKK, kurahisisha kazi ya walimu wanaofundisha
watoto wa darasa la kwanza na la pili pamoja na kuongeza ushiriki wa
jamii katika kuboresha elimu na hasa ujifunzaji wa stadi za KKK.
Alisema mpango huo utachangiwa sh. bilioni 150 ambazo zitaingizwa moja kwa moja kwenye mfuko wa elimu kupitia Wizara ya Fedha.
Alisema
maandalizi yote ya utekelezaji wa mpango huu yamekamilika ikiwa ni
pamoja na mtaala wa darasa la kwanza na darasa la pili, muhtasari wa KKK
kwa darasa la I & II, pamoja na Mwongozo wa Mwalimu wa kufundisha
kusoma kuandika na kuhesabu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, FEBRUARI 8, 2015.
EmoticonEmoticon