Serikali yajipanga kutumia nguzo za zege kusambaza umeme

February 09, 2015

Wataalam wa Sekta ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto), wakiwa katika mazungumzo na wawakilishi wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd (Kulia). Mazungumzo yalifanyika hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, jijini Dar es Salaam na yalihusu uanzishwaji wa Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya kusambaza umeme nchini.
Ujumbe kutoka Kampuni ya Sunshine Group Ltd, ukiwa katika mazungumzo na wataalam wa Sekta ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme nchini – Tanesco (hawapo pichani). Kampuni hiyo iliwasilisha mapendekezo (proposal) ya kuanzisha Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini.

Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (Kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd, Bw. Sun Tao aliyekuwa akitoa ufafanuzi wa jambo fulani, mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya Wataalam wa Wizara na wawakilishi wa Kampuni hiyo kuhusu uwezekano wa kuanzisha Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya kusambaza umeme nchini.

Na Veronica Simba

Serikali inaendeleza jitihada za kuachana na matumizi ya nguzo za umeme za miti na badala yake kutumia nguzo za zege ikiwa ni hatua mojawapo ya kuboresha huduma ya usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini.

Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki katika kikao baina ya uongozi wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd na wataalam wa sekta ya umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Katika kikao hicho, Kampuni ya Sunshine iliwasilisha mapendekezo (proposal) ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini.

Akieleza msimamo wa Serikali kuhusu mapendekezo hayo, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga alisema Serikali ina dhamira ya kutumia nguzo za umeme zilizotengenezwa kwa zege na kuachana na za miti zinazotumika sasa kutokana na manufaa yake.

Mhandisi Luoga aliyataja manufaa ya kutumia nguzo za zege kuwa ni pamoja na uimara wa nguzo husika. “Huwezi kulinganisha uimara wa nguzo za zege na hizi za miti tunazotumia hivi sasa. Nguzo za zege ni madhubuti na imara zaidi,” alisema.

Akifafanua zaidi, Mhandisi Luoga alisema, kutokana na uimara wa nguzo za zege, uhai wake ni wa muda mrefu kulinganisha na nguzo za miti.

“Uhai wa nguzo za zege ni kati ya miaka 70 hadi 100, wakati uhai wa nguzo za miti ni miaka 50,” alisema Luoga na kusisitiza kuwa sifa hiyo ya uhai mrefu wa nguzo za zege inazalisha manufaa mengine kwa Serikali na wananchi kwa ujumla endapo nguzo hizo zitatumika.

Akielezea manufaa yanayotokana na uhai mrefu wa nguzo za zege, Mhandisi Luoga alisema Serikali itatumia fedha kidogo kutokana na nguzo za zege kudumu kwa muda mrefu, tofauti na nguzo za miti ambazo uhai wake ni mdogo.

Aidha, faida nyingine za kutumia nguzo za zege, zilizotajwa na wataalam katika kikao hicho ni pamoja na kuwa rafiki wa mazingira ambapo huepusha ukataji wa miti.

Nyingine ni uwezo wake wa kutopitisha maji na kutoshika moto kwa urahisi (water and fire proof). Akihitimisha mazungumzo husika, Kamishna Luoga alisema Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na Kampuni hiyo pamoja na wawekezaji wengine wenye nia ya kutengeneza nguzo za umeme za zege ili kufikia makubaliano yatakayowezesha pande zote mbili kunufaika.

“Mkakati wetu ni kwa Tanesco kutengeneza nguzo za zege kwa matumizi ya ndani ya nchi lakini ni vema tukapata wawekezaji wengine watakaosaidia kutengeneza nguzo hizo kwani mahitaji ni makubwa sana,” alisema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »