Wakazi
wa mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika
daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi
mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jerry Silaa wakati akiongea kwenye
kilele cha sherehe za kutimiza miaka 38 ya chama hicho mkoani Lindi
zilizofanyika katika tawi la Mnazi Mmoja lililopo kata ya Mingoyo wilaya
ya Lindi mjini.
Silaa mbaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala alisema
iwapo mtu atajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura
atashiriki katika uchaguzi mkuu ujao hivyo basi wakati ukifika ni jukumu
la mabalozi kuwahimiza wananchi kujiandikisha ili wasipoteze haki yao
ya msingi ya kupiga kura.
Aidha Meya Silaa aliwapongeza wana CCM kwa ushindi wa asilimia
77 walioupata wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na
vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana na kuwataka kuwa makini
katika kuteua viongozi wanaokubalika na wananchi na kuachana na makundi
yanayokibomoa chama hicho kwa kufanya hivyo itawawezesha kupata ushindi
wa kishindo katika uchaguzi ujao.
Kwa upande wa vijana aliwahimiza kujishughulisha katika shughuli
za kimaendeleo ili waweze kujipatia maendeleo kwani mkoa wa Lindi uko
katika dira ya maendeleo kwa kuwa na ardhi yenye rutuba, barabara nzuri
na gesi.
Silaa alisisitiza, “Nawashauri vijana wenzangu mjiunge na CCM
chama kinachowasaidia vijana kuwaletea maendeleo ukilinganisha na vyama
vingine vinavyowapotezea muda na kurudisha nyuma maendeleo yenu”.
Alikipatia kikundi cha Zamira ambchi kinajishughulisha na kilimo
na ujasiriamali shilingi laki tano ili ziweze kuwasaidia kuinua mtaji.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete alisema sherehe hizo zina umuhimu wa
kipekee kwa wana CCM kwani zimeangukia mwaka wenye matukio muhimu na
makubwa kwa nchi ambayo ni kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na
uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
alisema mwaka 2015 ni mwaka wa kuhitimisha utekelezaji wa Ilani ya CCM
ya mwaka 2010-2015 ambapo Chama hicho kiliwaomba wananchi wakichague ili
kiwafanyie kazi watanzania ambao walikiamini na kukichagua.
“Matokeo yake watanzania wameyaona , miundombinu ya barabara,
shule na vyuo vimejengwa na watoto wengi hivi sasa wapo mashuleni.
Huduma za afya zimeboreka kwa kujengwa Hospitali, vituo vya afya na
Zahanati”.
Lakini hata kwa yale ambayo hayakuwepo kwenye Ilani na yalikuwa
ni matakwa ya wananchi chama chetu sikivu hakikusita kuyakubali kwani
yalikuwa ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa na vizazi vyetu”, alisema Mama
Kikwete.
Kuhusu Katiba inayopendekezwa MNEC huyo alisema itapigiwa kura
ya maoni mwaka huu mwezi wa nne hivyo basi aliwataka wanaCCM na
watanzania wote kwa ujumla kuipigia kura ya ndiyo katiba pendekezwa
kwani inakidhi matakwa ya watanzania kwa kuwa imegusa katika maeneo
yote.
Akiwasalimia wananchi waliohudhuria sherehe hizo Mkuu wa wilaya
ya Lindi Dkt. Nassoro Hamidi aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto
walioandikishwa darasa la kwanza na wale waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza wanaenda shule kuanza masomo ili waweze kupata elimu
itakayowasaidia katika maisha yao.
Katika kilele cha sherehe hizo zilizoenda sambamba na wiki ya
Chama na Jumuia zake kauli mbiu yake ni Umoja ni ushindi, Katiba yetu,
Taifa letu jumla ya wanachama wapya 448 walijiunga na chama hicho ambapo
saba walitoka vyama vya upinzani, Chama cha Wananchi (CUF) watano na
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wawili