Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – aliyekuwa Lindi
Wananchi
wa mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya ndiyo
katiba inayopendekezwa kwani ni bora na imegusa maeneo yote kwa ajili
ya maendeleo ya Watanzania.
Rai
hiyo imetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na wananchi waliohudhuria sherehe ya kushangilia ushindi wa
uchaguzi wa Serikali za mitaa katika mtaa wa Ruaha kata ya Mingoyo
wilayani humo.
Katika
uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwishoni
mwa mwaka jana wananchi wa mtaa wa Ruaha waliwachagua Mwenyekiti na
wajumbe wote watano kutoka Chama Cha Mapinduzi.
Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema katiba
inayopendekezwa imeangalia maeneo yote yanayomgusa binadamu ikiwa ni
pamoja na haki za wanawake na watoto, watu wenye mahitaji maalum
wakiwemo walemavu na wazee.
“Katiba
iliyopo sasa ilitungwa na baadhi ya watu waliokuwa madarakani kwa
wakati ule na haikuwahusisha wananchi, lakini hii inayopendekezwa
wananchi wameshiriki kuitunga kwa kutoa maoni yao”, alisema Mama
Kikwete.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza aliwahimiza wananchi
hao kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wasipoteze
haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Mahiza
alisema kama kuna watu waliojiandikisha katika miaka ya nyuma wabebe
vitambulisho vyao ili viweze kunukuliwa na kwa wale wenye umri wa
kuanzia miaka 18 wakajiandikishe na walio na umri wa chini ya hapo
wasijiandikishe.
Aliwaasa wananchi hao kutokubali wageni waliokaa katika maeneo yao kwa kipindi cha chini ya miezi sita kujiandikisha.
Akisoma
taarifa ya CCM tawi la Ruaha Mohamedi Ngashona ambaye ni mjumbe alisema
viongozi hao wamejipanga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa
mtaa huo ambazo ni uharakishaji wa ujenzi wa zahanati, ukarabati wa
vyumba vya madarasa na ujenzi wa nyumba za walimu.
Kuwatambua
kaya maskini na wazee kwa kuwapatia huduma muhimu, uimarishaji wa
barabara ya kutoka Mnazimmoja hadi Ruaha na utekelezaji wa sera ya umeme
vijijini hasa vilivyopitiwa na mradi wa bomba la gesi.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama 43 walijiunga na chama hiyo kati yao wanne walitoka Chama cha Wananchi CUF .
EmoticonEmoticon