Kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Zanzibar na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL
ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla wakitiliana saini mkataba wa
makubaliano ya kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa
Zanzibar Nchini India. (Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar)
Kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Zanzibar na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL
ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla wakikabidhiana mkataba wa
makubaliano ya kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa
Zanzibar Nchini India baada ya kumaliza kusaini. (Picha na Makame
Mshenga Maelezo-Zanzibar)
Katibu
Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Nd. Saleh Ramadhan Ferouz
akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa
tukio hilo. (Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar)
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar na Wa 3
kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India
Nd. Jilesh H. Babla na viongozi wengine kutoka Wizara ya Habari pamoja
na Kamisheni ya Utalii Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja.
(Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar)
……………………………………………………………………………….
(Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar)
……………………………………………………………………………….
Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Wizara ya Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar imetia saini mkataba wa makubaliano ya
kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa Zanzibar Nchini
India.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Nd. Ali Mwinyikai wakati wa kutia saini Mkataba huo katika
ukumbi wa Wizara hiyo iliyopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mkataba huo umetiwa saini tarehe
17/02/2015 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Nd. Ali Mwinyikai na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh
H. Babla.
Katibu huyo amesema kuwa
uanzishwaji wa ofisi ya utalii nchini India haukuja kwa bahati mbaya ila
ni utekelezaji wa ilani na malengo yaliyopangwa na kutekelezwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyopo madarakani kwa upande wa sekta
ya Utalii kwa lengo la kuitangaza zaidi Zanzibar kiutalii.
Amesema ofisi hizo zitafanya kazi
kama mabalozi wa kuutangaza Utalii wa nchi zao kwa kuwapatia habari
watalii wote ambao wana nia ya kuzitembelea nchi husika pamoja na kutoa
ushawishi mkubwa utakaowafanya wananchi wa nchi hizo kuwa na maamuzi
sahihi ya kuzitembelea nchi hizo.
Aidha Katibu huyo amesema kuwepo
kwa ofisi za Utalii nchini India itasaidia kujenga uhusiano mzuri na wa
kudumu baina ya Zanzibar na wadau mbalimbali wa Utalii walioko nchini
India jambo ambalo linakosekana katika masoko yaliyopo hivi sasa ispokua
soko la Itali.
“Tuna kila sababu za Zanzibar nayo
kutumia mfumo huu wa utangazaji wa Utalii kwani unaweza kuleta tija
kubwa kwa haraka ukilinganisha na mifumo mengine ya utangazaji”,
ameeleza Katibu Mwinyikai.
Amesema mpango huo umelenga kuimilikisha Sekta ya Utalii kwa
wanachi wote wa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa uwepo wa sekta hiyo
unawafaidisha wananchi wa Zanzibar Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni.
Ametanabahisha kuwa kupanuka kwa
wigo wa masoko ya Utalii kutaongeza kazi ya utekelezaji wa dhana ya
Utalii na kuondokana na utegemezi wa soko la Ulaya ambalo linatishia
uhakika wa kuwepo kwake kutokana na athari za Kiuchumi na Kifedha
zinazojitokeza siku hadi siku.
Nd. Mwinyikai amefahamisha kuwa
kutokana na hali hiyo Serikali ya Zanzibar imeamua kuongeza nguvu na
kubadilisha mikakati ya utafutaji wa masoko mengine ikiwa ni pamoja na
yale yanayochipukia yakiwemo ya Nchi za China, India, Urusi na Uturuki.
Nae mkurugenzi mtendaji wa kampuni
ya Jihil Enterprises ya India ambae pia ni mzaliwa wa Zanzibar anaeishi
Mumbai India Nd. Jilesh H. Babla amesema ameamua kuwa wakala wa Utalii
wa Zanzibar Nchini India kwa lengo la kuitangaza Zanzibar kiutalii kwani
Zanzibar ina vivutio vingi vya Kiutalii zikiwemo Fukwe na Mandhari
mazuri ya Kisiwa hicho pamoja na sehemu za kihistoria.
Amesema ameamua maamuzi ya
kizalendo kuwa Wakala wa Zanzibar Nchini India kwani hadi sasa hakuna
wazalendo wanaoishi nje ya Nchi waliyojitikeza kufanya kazi hiyo pamoja
na kuvitaka vyombo vya habari Zanzibar kufikisha ujumbe uliyo sahihi kwa
wananchi juu ya Utalii wa Zanzibar ili kukuza Utalii wa nchi na hatimae
kupelekea kukua kwa uchumi wa nchini.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya
Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dr. Ahmada H. Khatib amesema wazo la kuwa
na Ofisi ya Utalii Nchini India lilitokana na matokeo ya ziara rasmi ya
Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
aliyoifanya Nchini China na India tarehe 27/05/2013 hadi 02/06/2013
ambayo ilijumuisha Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Amesema pamoja na kuwa takwimu za
idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar bado zinakumbana na changamoto
za kutokuwa sahihi hata hivyo idadi ya sasa inaonyesha kuwa India hutoa
watalii zaidi ya 98,000 kwa kila mwaka hivyo ipo haja ya kuwepo kwa
wakala wa Utalii wa Zanzibar Nchini humo.
Amefahamisha kuwa makisio ya jumla
ya kuendesha Ofisi hiyo Mjini Mumbai, India inakadiriwa kufikia zaidi
ya Dola 100,000 za kimarekani kwa Mwaka ambapo Dola zipatazo 27,000 ni
za kuendeshea Ofisi hiyo kila mwezi.
EmoticonEmoticon