Na Mwandishi Wetu, Handeni
TAMASHA la
Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu, sasa litafanyika Desemba 20, badala ya Desemba
13, kama ilivyotangazwa hapo awali, huku sababu kubwa ikiwa ni kuwaachia
Watanzania washiriki katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa,
utakaofanyika Jumapili ya Desemba 14 nchini kote.
Mratibu
Mkuu wa Tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, pichani akizungumza jambo
katika tamasha la mwaka jana lililofanyika kwa mafanikio makubwa
wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumzia hilo leo mjini Handeni, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kwamba
hatua ya kusogeza mbele kwa wiki moja, ni kutokana na mguso wa tukio lenyewe na
nia ya kuwashirikisha Watanzania wote ili kuliweka tamasha lao katika kiwango
cha juu.
Alisema kuwa
Desemba 13 ni siku ya mwisho kwa kampeni za ugombea uenyekiti wa serikali za
mitaa, vitongoji na mitaa, hivyo kwa kushauriana na jeshi la Polisi wilayani Handeni,
wamekubaliana kulifanya Desemba 20.
“Tumeangalia
mambo mengi sana hadi kukubaliana lifanyike Desemba 20, ikiwa ni kukosekana kwa
wengi, wakiwamo Wakurugenzi ambao kimsingi wao ndio wasimamizi wa uchaguzi
katika maeneo mengi.
“Tunaamini
kwa kufanyika Desemba 20, tamasha litakuwa kwenye mvuto pamoja na kukwepa
malalamiko kwa baadhi ya wanasiasa ambao huenda wangelalamika endapo lolote
lingetokea huku wao kushindwa uchaguzi wao,” alisema Mbwana.
Mbwana
alitumia muda huo kuwaomba radhi wadau wote, wakiwamo wasanii, wadhamini na
wale waliokuwa wamepanga kutembelea Handeni Desemba 13, huku akiwataka safari
yao ifanyike kwa ajili ya Desemba 20, ukizingatia kuwa wote wanaweza kushiriki
chaguzi zao na kupata muda mkubwa wa kutembelea wilayani Handeni na mkoa mzima
wa Tanga kumaliza mwaka wao vizuri.
Wadhamini tamasha
hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans,
SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha
‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film
Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and
Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.
EmoticonEmoticon