MIKOA MITANO YATAKIWA KUWASILISHA USAJILI COPA 2014
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka mikoa mitano
kuwasilisha usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya mashindano ya Taifa ya Copa
Coca-Cola 2014 kabla ya Desemba 5 mwaka huu.
Mikoa hiyo ambayo haijawasilisha usajili wake hadi sasa kwa ajili
ya michuano hiyo inayoanza Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Arusha,
Dodoma, Katavi, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Simiyu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano ya michuano hiyo, mkoa ambao
hautawasilisha usajili wake kwa ajili ya uhakiki wa umri wa wachezaji utakaonza
Desemba 10 mwaka huu utaondolewa katika fainali hizo zitakazomalizika Desemba
20 mwaka huu.
Wachezaji watakaobainika kuzidi umri hawataruhusiwa kushiriki
katika michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 15.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya michuano kuhusu idadi ya wachezaji, kila timu
inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 20 na wasiopungua 16.
Hivyo, kila timu inatakiwa kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya
wachezaji, kwani kikanuni wakipungua 16 itaondolewa kwenye mashindano.
Timu 16 kwa upande wa wavulana zitashiriki katika fainali hizo
wakati kwa upande wa wasichana ni timu nane. Mikoa iliyoingiza timu za
wasichana kwenye fainali hizo ni Arusha, Dodoma, Ilala, Kinondoni, Mbeya,
Mwanza, Temeke na Zanzibar.
MANDAWA
MCHEZAJI BORA WA VPL NOVEMBA
Mshambuliaji wa timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera amechaguliwa
kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo
atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji
Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino
atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.
Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa
mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar
itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI
YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHI
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele
kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika
tarehe itakayotangazwa baadaye.
TFF imepokea maombi ya zaidi ya washiriki 40 kwa ajili ya kozi
hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi
zilizopo, FIFA itafanya mchujo wa washiriki.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon