Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango),
Bi Joyce Mkinga (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati alipokuwa akitoa taarifa ya kufanyika kwa Mkutano wa Maafisa Mipango unaotarajiwa kufanyika Mwezi wa Oktoba mwaka huu. Kulia ni Mchumi Mkuu (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bw. Omary Juma.
***********************************************
Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango ipo katika maandalizi ya mkutano wa mwaka wa wachumi
na maafisa mipango unatarajiwa kufanyika Oktoba 2014 jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa uchumi na
mipango hapa nchini.
Mkutano
huu ambao ni wa kitaalamu unawakutanisha
wataalamu mbalimbali kutoka tasnia za mipango, uchumi, takwimu na maendeleo,
wenye wajibu wa kusimamia uchumi na mipango ambao hukutana kwa ajili ya
kujadili na kubadilishana uzoefu juu ya sera, mipango na kujenga mtandao wa
masuala ya maendeleo ya kitaaluma.
Mkutano
huu unatoa fursa kubwa ya kuwakutanisha kwa pamoja wataalamu hao na kujenga
uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Pia
hutoa fursa za kujadiliana kwa pamoja juu ya mafanikio na njia za kukabiliana
na changamoto kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi kwenye masuala hayo. Mkutano
huo ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa kada hizi kwa minajili ya kusukuma
gurudumu la maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Kwa
kutilia mkazo masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayojitokeza hivi sasa, mkutano
wa mwaka huu utajikita katika kujadili masuala yafuatayo;
i) Maendeleo ya Tasnia
ya Wapanga Mipango (wachumi, maafisa mipango na watakwimu);
Mkutano utajadili fursa, na changamoto zilizopo katika
kuleta maendeleo katika nchi. Huko nyuma
kada hizi zilikuwa zinaratibiwa na iliyokuwa Wizara ya Mipango Uchumi na
Uwezeshaji. Kwa sasa watakuwa chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango. Hatua hii itarahisisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya nchi.
ii) Maandalizi ya
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/16 – 2020/2021);
Utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo
2011/12 – 2015/16) unaendelea na tayari Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango imeanza
kufanya mapitio ya utekelezaji wake ili kujua mafanikio na changamoto. Hivyo,
katika mkutano huo wapanga mipango wanaandaliwa waweze kuanza kufanya
maandalizi kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo (2015/16 – 2020/21).
iii)
Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma;
Serikali imeandaa mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji
katika sekta ya Umma, lengo likiwa kuimarisha utendaji, ufanisi na uwajibikaji
katika matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya miradi na
program za maendeleo.
iv)
Jinsi ya Kujiandaa na Uchumi wa Gesi
Mkutano utajadili ni kwa jinsi gani Tanzania inajipanga kufaidika
na rasilimali ya gesi asilia. Kwa kifupi masuala ya yanayohusu uwekezaji katika
gesi asilia, usimamizi na jinsi ya kutumia rasilimali na menejimenti ya mapato
yatokanayo na gesi, pamoja na ushiriki wa wananchi katika fursa mbalimbali
zinazotokana na ujio wa gesi hiyo. Utayarishaji wa wataalam katika eneo hilo la
gesi husani vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na kadhalika.
Washiriki
wa mkutano huu ni pamoja na wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango
kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na
taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na
uchumi.
Mkutano
wa mwisho wa mwaka wa maafisa mipango ulifanyika mkoani Morogoro tarehe 12
Machi 2010 ambapo uliandaliwa na Wizara ya Fedha. Mada nne zilizowasilishwa na kujadiliwa zilikuwa
ni;
i.
Wajibu wa wataalamu wa mipango katika Maendeleo ya Uchumi:
Mipango ya Kiuchumi, Utekelezaji na Uandaaji wa Taarifa;
ii.
Soko la Pamoja la
Afrika ya Mashariki;
iii.
Ujasiriamali na
Usimamizi wa Biashara kwa Wafanyabiashara Wadogo na Wakati; na
iv.
Ufanisi wa Uwekezaji
kutoka nje katika Uchumi wa Tanzania
Imetolewa na:
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
EmoticonEmoticon