Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara
Azam fc wameanza ligi kwa kishindo baada ya kuitandika Polisi Morogoro 3-1
katika mchezo wa ufunguzi wa msimu wa 2014/2015 uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City kama
ilivyokuwa msimu uliopita, wameanza ligi kwa kutoa suluhu pacha ya bila
kufungana (0-0) katika dimba lao la Sokoine jijini Mbeya dhidi ya JKT Ruvu.
Afisa habari wa Mbeya City, Dismas Ten amesema mechi
ilikuwa ngumu kwa timu zote na matokeo hayo ni ya kawaida katika mpira, lakini
benchi la ufundi litakaa chini kufanya marekebisho.
Katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, bao pekee
la Ramadhani Pela limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Mgambo JKT dhidi ya Kagera
Sugar iliyosafiri kutoka Kaitaba.
Kikosi cha Mbeya City fc
Katibu mkuu wa klabu hiyo, Antony Mgaya amesema kuwa
wamefurahishwa na ushindi huo licha ya kupata upinzani wa kutosha, hivyo
wanajipanga kwa mechi ijayo ili kuendeleza wimbi la ushindi.
Katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani,
Tanzania Prisons ‘Wajelajela’ wamewatandika wenyeji wa uwanja huo, Ruvu Shootings
mabao 2-0.
Huko Kambarage mkoani Shinyanga, Stand United
wakiwa nyumbani wametandikwa mabao 4-1 na Ndanda fc kutoka mkoani Mtwara.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Ndanda fc
walikuwa mbele kwa mabao 3-1 na kipindi cha pili wakaongeza bao la nne.
Katibu mkuu wa Ndanda fc, Seleman Kachele amesema
walitawala mchezo huo na ni mwanzo mzuri kwao.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi moja kupigwa ili kukamilisha mzunguko wa kwanza ambapo wekundu wa Msimbazi Simba watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuivaa Coastal Union.
EmoticonEmoticon