TANGA.
KATIBU MKUU wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM),
Abdulrahamani Kinana anatarajiwa kuwasili mkoani Tanga Septemba 23 mwaka huu
kwa ajili ya ziara yake ya kutembelea majimbo 11 mkoani Tanga na kuzindua miradi
mbalimbali ya maendeleo kisha kuweka mawe ya msingi.
Akizungumza na TANGA RAHA OFISINI KWAKE, Katibu wa
CCM Mkoa wa Tanga, Shija Othumani alisema katibu huyo atapokelewa wilaya ya
Handeni akitokea mkoani Pwani ambapo baadaye atazindua miradi ya kuweka mawe ya
msingi eneo la Mkata pamoja na kushiriki kwenye mradi wa maji, ujenzi wa
maabara kwenye shule za sekondari wilayani humo.
Alisema kuwa licha ya hayo atashiriki kwenye ujenzi
wa matawi ya chama na majengo ya makao makuu kwa baadhi ya kata
atakazozitembelea ambapo akiwa wilayani humo atashiriki kwenye ujenzi wa tawi
la Kwenjugu mashariki.
Aidha alisema kuwa akiwa wilayani Korogwe, Kinana
ataweka jiwe la msingi ofisi ya Chama hicho Kata ya Mashewa ikiwemo kufanya
mikutano ya ndani pamoja na kuzungumza kupitia halmashauri kuu za wilaya.
Aliongeza kuwa licha ya kufanya kazi hizo, Katibu
huyo atashiriki kwenye kazi mbalimbali ikiwemo za kufyetua matofauli kwa ajili
ya ujenzi wa vyumba vya maabara kwenye wilaya ambavyo zimepangwa kufanya hivyo.
“Katibu Mkuu
Kinana atawasili mkoani hapa Septemba 23 mwaka huu na atapokelewa kata ya Mkata
wilayani Handeni hivyo wananchi na wakazi wa maeneo jirani hakikisha mnajitokeza
kwa wingi kumlaki kiongozi huyo “Alisema
Mwisho.
EmoticonEmoticon