MAKORORA WAFANYIA BIASHARA CHAKULA CHA MSAADA.

May 01, 2014


MBUNGE wa Korogwe vijijini Stephen Ngonyani juzi aliiweka kikaangoni serikali ya kijiji cha Makorora akihoji uhalali wa kuwauzia wananchi chakula cha msaada kwa kwa bei ya Tsh
100/= kwa kilo badala ya Tsh 50/= zilizoelekezwa na serikali vitendo ambavyo vimewakera wananchi.

Hatua hiyo ya kuhojiwa kwa serikali ya kijiji hicho iliyotakiwa kutoa maelezo ilikuja baada ya risala kusomwa kwa mbunge huyo na mwenyekiti wa vijana wa tawi la CCM Ringo Mjenga aliyesema,haki haikutendeka kutokana na kuuziwa mahindi ya msaada kwa bei iliyo kinyume na  utaratibu.

Baada ya mwenyekiti wa serikali Aziza Shemkunde kujitetea kuwa  kutokuwepo wakati maamuzi yakifanywa ili kuongeza nguvu ya kupata fedha za kusukuma miradi mingine,mbunge Ngonyani alisema ameisamehe serikali hiyo kwa vile ni kosa la kwanza akiwaasa kutorudia makosa.

“Kuhusu chakula cha msaada serikali ya kijiji ilikosea,kwa kuwa mwenyekiti wa kijiji ni mgeni nimemsamehe vinginevyo ningeondoka naye”alisema Ngonyani huku akitoa Tsh 80,000/= ili ziweze kurejeshwa kwa wananchi ambao walinunua chakula hicho kwa bei ya Tsh 100/=.

Aidha alimtaka afisa mtendaji wa kijiji hicho Bakari Zayumba kusimamia vizuri urejeshwaji wa fedha hizo kwa waathirika wa tukio hilo bila ya kuwepo kwa malalamiko ya aina yeyote ile miongoni mwao.

Pamoja na kutoa fedha hizo ili kuweza kurejeshwa kwa wananchi ambao waliuziwa chakula kwa bei kubwa kama walivyomlalamikia mbunge huyo aliwasisistiza viongozi kutokukiuka maagizo yaliyowekwa na serikali.

Mbali na maelekeo hayo Ngonyani aliwaasa wananchi wa kijiji hicho cha Makorora kutokushabikia mambo kwa kuwasilishabaadhi ya kero ambazo hawana ushahidi nazo huku akiwataka kuendelea kumpatia ushirikiano yeye pamoja na diwani wao njia itakayosaidia kuharakisha maendeleo.

Vilevile alikemea vikali tabia tabia za baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kushiriki misalagambo kwenye miradi ya maendeleo ambapo alimtaka afisa mtendaji wa kijiji hicho kuendelea kuona hamasa watu kushiriki kazi hizo sanjari na kuwashughulikia wakaidi.

“Atakayezuia misalagambo jina lake liorodheshwe lifikishwe kwenye vyombo vya kisheria,ili miradi yetu ifanye vizuri tuna haja wote kushiriki pindi tunapohitajika,kusiuwepo kwa visingizio”alisema Ngonyani  akisisitiza umuhimu wa viongozikukosoana wakitumia vikao.

Akielezea sakata hilo Afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Kakulu Lugembe alisema ni kinyume cha Sheria Serikali ya kijiji kujipangia bei ya chakula cha msaada kinyume na mwongozo wa bei ya Serikali na kuahidi kulifuatilia suala hilo kwa hatua zaidi


Mbunge wa Korogwe vijijini Stephen Ngonyani akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Makorora kata ya Magoma mwishoni mwa wiki. (Picha na mtandao)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »