Mkuu wa mkoa wa Tanga Luteni Mstaafu Chiku
Gallawa jana aliongoza mamia ya wakaazi wa kijiji cha Kwamzindawa kilichopo
kata ya Mnyuzi, Korogwe vijijini kutundika mizinga ya nyuki pembezoni mwa milima
inayopakana na hifadhi ya asili ya Amani katika
kuadhimisha siku ya kutundika
mizinga nchini ambapo kitaifa shughuli hiyo ilifanyika mkoani Katavi .
Maadhimisho hayo ya kimkoa yaliyoratibiwa na Wakala
wa misitu Tanzania (TFC) kwa ushirikiano na Halmashauri ya wilaya ya Korogwe
yalifanikisha utundikaji wa mizinga 45 iliyotolewa na TFC shughuli iliyofanywa
kwa umakini na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano na Wananchi wakiongozwa na
Mkuu wa mkoa.
Katika hotuba yake mara baada ya zoezi hilo
Mkuu wa mkoa alikipongeza kikundi cha ufugaji nyuki cha Malkia cha kijijini
hapo ambacho ndiyo kimekuwa chachu ya kuendeleza ufugaji nyuki waliouanzisha kwa jitihada zao binafsi na
baadaye kupatiwa msaada wa vifaa vya kufugia na kurinia asali ikiwemo mizinga
hiyo.
Gallawa aliongeza kuwa ni vyema kikundi hicho
kikajenga mtandao wa ulinzi na utunzaji wa mazingira ili kuwavutia zaidi nyuki
kuingia katika mizinga hiyo na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuwaandalia
mafunzo ya kitaalamu wafugaji hao ili ufugaji huo ukue na kufikisha mizinga 100
hatimaye uweze kuwa na tija kwenye uchumi endelevu.
“Agizo la mkoa ni kila kikundi cha ufugaji
nyuki kuwa na mizinga 100 hapo ndipo mnaweza kuona tija ya ufugaji nyuki ambao mtaji
na uwekezaji wake ni mdogo,lakini faida ni kubwa.” Aliongeza Gallawa.
Kadhalika aliwashauri wafugaji hao kulima zao
la alizeti ambalo huvutia nyuki hivyo itapelekea kupata faida mara zaidi
hatimaye kufanikisha kipaumbele cha mkoa cha kumfanya mkazi wa Tanga kuongeza
pato hadi kufikia Tsh ml 1.5 kwa mwaka.
Awali katika risala yao iliyosomwa na Fatuma
Kipara, kikundi cha ufugaji nyuki cha Malkia walimweleza Mkuu wa mkoa kuwa wanakabiliwa
na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa sekta ya nyuki jambo linalowaathiri kwa
kuwa hawatembelewi mara kwa mara.
Naye
Afisa nyuki wa wilaya Vicent Mhezi, akisoma taarifa ya ufugaji nyuki alisema Wilaya ina vikundi
vya ufugaji wa nyuki 38,vyenye wanachama 602, vikundi vilivyosajiliwa ni 13 na kuongeza kuwa
Korogwe imefanikiwa kuanzisha ofisi ya
usindikaji wa Mazao ya Nyuki iliyopo Bungu,ambapo kwa mwaka 2013,wamefanikiwa
kusindika asali lita 500 yenye thamani ya Tshs 5,000,000/-
Diwani wa kata ya Mnyuzi Rajab Muhidin akitoa maelezo ya awali kuhusu kata yake kwa Mkuu wa Mkoa. |
Afisa Nyuki wilaya Vicent Mhezi akieleza teknolojia iliyotumika kutengeneza mizinga hiyo kwa Mkuu wa Mkoa |
Shughuli ya kutundika mizinga ikiendelea mara baada ya Mkuu wa Mkoa kuzindua zoezi hilo.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Edith Mallya akiungana na Mkuu wa Mkoa katika kutundika mizinga
Baada ya "tundikatundika" , tuliacha eneo hilo likionekana namna hii
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Luten Mstaafu Chiku Gallawa akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Mzindawa
Wananchi wa Mzindawa walioshiriki tukio hilo wakimsikiliza Mh.Mkuu wa Mkoa
Mwisho Mkuu wa Mkoa alihitimisha shughuli hiyo kwa kutembelea banda la
maonesho la kikundi cha Malkia kujionea mazao yatokanayo na Nyuki
EmoticonEmoticon