HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2014/2015

May 07, 2014

prime-minister

UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.
  1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa  naomba  nichukue  fursa  hii kutoa salamu za pole  kwako  na kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01 Januari, 2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze, ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape pole Wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013. Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa Wabunge na  Wananchi  wote  waliofiwa  na ndugu na jamaa zao kutokana na majanga na matukio mbalimbali tangu  nilipowasilisha  Bajeti  yangu  ya  mwaka  2013/2014.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina! Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

MAANDALIZI YA BAJETI

  1. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti ambao unatuwezesha kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka.  Taarifa za awali zinabaini kwamba utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa kazi zilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwa kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi   ya   Chama   Cha   Mapinduzi  ya  mwaka  2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN). Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kipaumbele  iliyoainishwa  kwenye  mipango  hiyo  ya  Kitaifa ili kuleta maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa Tanzania.
  1. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni kubwa na ambayo imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.

HALI YA SIASA

  1. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu  yao. Nchi  yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito ambapo tunaandika Katiba Mpya itakayoweka mustakabali wa  mwelekeo wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo ambayo baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni.  Nawaomba tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.

  1. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013. Aidha, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata usajili wa muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote vya siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.

ULINZI NA USALAMA

Usalama wa Raia

  1. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi nzima. Vikundi hivyo vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini kutoka Asilimia 4.3 mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia kupungua kwa makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012 hadi makosa 560,451 mwaka 2013.

Mauaji ya Wanawake

  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8) wameuawa kikatili katika Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani Butiama. Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana na kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inalaani vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote. Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya mauaji ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13 wamefikishwa mahakamani.  Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe wito kwa wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo wake.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »